NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
MWANAFUNZI wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Abilai Kalela, ambaye ni Mhitimu wa Diploma ya Ufundi Umeme wa Magari, amebuni mfumo maalum wa kiteknolojia unaolenga kudhibiti vyombo vya usafirishaji kama magari, bajaji na maroli dhidi ya kuzidisha mizigo, hatua inayolenga kupunguza ajali za barabarani na kulinda vyombo hivyo dhidi ya uharibifu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam Mei 8, 2026 katika maonesho ya wahandisi vijana, Kalela amesema ubunifu huo umejikita katika kuhakikisha magari ya mizigo hayabebi mizigo inayozidi uwezo wake, hali ambayo imekuwa ikichangia ajali pamoja na kuharibu injini za magari hayo.
Amesema licha ya kuwepo kwa utaratibu rasmi wa ubebaji wa mizigo, bado baadhi ya madereva wamekuwa wakikiuka viwango vinavyotakiwa kwa kupakia mizigo kupita kiasi.
Kwa mujibu wa Kalela, mfumo huo una uwezo wa kutambua mzigo uliozidi mara moja na endapo utafungwa kwenye gari au chombo kingine cha moto, hautaruhusu chombo hicho kuondoka hadi pale mzigo utakapopunguzwa na kufikia kiwango kinachoruhusiwa.
Ameeleza kuwa pamoja na kusaidia kuongeza usalama barabarani, mfumo huo pia utawasaidia madereva kuepuka faini zinazotokana na kubeba mizigo kupita kiwango kinachokubalika.
Naye Ofisa Uhusiano wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Juma Mandai, amesema changamoto ya madereva kupakia mizigo kupita uwezo wa vyombo vya usafirishaji imekuwa ikisababisha hasara kubwa kwa wamiliki wa magari, maroli na bajaji, pamoja na kuchangia uharibifu wa barabara.
Ameongeza kuwa kupitia ubunifu wa Kalela, changamoto hiyo inaweza kupungua kwa kiasi kikubwa kwa kusaidia vyombo vya usafirishaji kudumu kwa muda mrefu na kupunguza gharama za matengenezo.
Mandai amesema katika kuhakikisha bunifu hizo za vijana zinaleta tija chuo hicho kwa kushirikiana Tume ya Vyuo Vikuu na Elimu ya Juu ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imekuwa ikihakikisha bunifu za wanafunzi zinaendelezwa ili ziweze kutoa suluhisho la changamoto mbalimbali katika jamii.
Aidha Mandai amesema chuo hicho kinaendelea kuwajengea uwezo wanafunzi wao wa kubuni miradi yenye lengo la kutatua changamoto mbalimbali katika jamii.




