NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
MKUU wa Tawi la Mafunzo Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Brigedia Jenerali Peter Mnyani amesema Michuano ya Kombe la Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele, imefanyika kwa weledi mkubwa na kufanikisha lengo la kuibua vipaji vya michezo pamoja na kuimarisha afya za vijana wanaohudumu katika jeshi hilo.
Akizungumza leo Juni 23,2026 jijini Dar es Salaam wakati wa kufunga michuano hiyo kwa niaba ya Mkuu wa JKT, Brigedia Jenerali Mnyani alisema mashindano hayo yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kutambua na kuendeleza vipaji vya wanamichezo watakaoiwakilisha JKT katika mashindano mbalimbali ya kijeshi na kitaifa.
Alisema mbali na kuibua vipaji, michuano hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kukuza nidhamu, uzalendo, mshikamano na ari ya kufanya kazi kwa pamoja miongoni mwa vijana wa JKT, mambo ambayo ni muhimu katika kujenga taifa imara.
“Michuano hii imeonesha uwezo mkubwa wa vijana wetu katika michezo mbalimbali na imeendelea kuwa sehemu ya kutengeneza wanamichezo bora watakaoiwakilisha JKT katika ngazi tofauti za mashindano,” alisema Brigedia Jenerali Mnyani.
Aidha, aliwataka wanamichezo waliochaguliwa kupitia mashindano hayo kuendelea kuvikuza na kuviboresha vipaji vyao ili waweze kufikia viwango vya juu zaidi vya ushindani na kuiletea heshima JKT pamoja na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Elimu, Michezo, Sanaa na Utamaduni JKT, Kanali Amos Mollo alisema mashindano hayo yamehusisha mamia ya wanamichezo kutoka vikosi mbalimbali vya JKT nchini, jambo lililowezesha kutambuliwa kwa vipaji vitakavyounda timu za jeshi hilo katika mashindano yajayo.
Kanali Mollo alisema wanamichezo waliofanya vizuri watajumuishwa katika timu za JKT zitakazoshiriki michuano mbalimbali ikiwemo CDF Cup na michezo ya majeshi, huku akisisitiza kuwa michezo imeendelea kuwa nyenzo muhimu ya kujenga afya na kuimarisha uwezo wa vijana.
Naye Kamanda wa Kikosi cha Mgulani JKT, Kanali Ernest Sambila alisema mafanikio yaliyopatikana katika mashindano hayo yametokana na maandalizi mazuri, ushirikiano wa viongozi wa ngazi mbalimbali pamoja na nidhamu iliyoonyeshwa na washiriki wote tangu kuanza hadi kumalizika kwa michuano hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano JKT, Meja Janeth Mkamba alisema mashindano hayo yamefanyika kwa weledi mkubwa na kuendelea kuimarisha taswira ya JKT kama taasisi inayowekeza katika maendeleo ya vijana kupitia michezo.
Alisema michezo imeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kujenga taifa lenye vijana wenye afya bora, umoja, mshikamano na uzalendo, huku JKT ikiendelea kutumia michezo kama sehemu ya malezi na maendeleo ya vijana nchini.
Michuano ya Kombe la Mkuu wa JKT imekuwa ikifanyika kila mwaka ikiwa na lengo la kuimarisha afya za vijana, kuibua vipaji vya michezo na kuandaa wanamichezo watakaoiwakilisha JKT katika mashindano mbalimbali ya kitaifa na kijeshi

