NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limezindua rasmi huduma mpya ya intaneti yenye kasi kubwa ijulikanayo ‘TTCL Faiba Supersonic Experience, Kasi Balaa’, hatua inayolenga kuharakisha mageuzi ya kidijitali na kuwapa Watanzania huduma bora zaidi za mawasiliano.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo, Mkurugenzi wa Biashara TTCL, Vedastus Mwita amesema kuwa tukio hilo linaashiria mwanzo wa hatua mpya katika safari ya maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano nchini, huku TTCL ikiendelea kuongoza juhudi za kuimarisha miundombinu ya mawasiliano na kutoa huduma za kisasa kwa wananchi.
Amesema TTCL imeendelea kuwekeza katika ubunifu na upanuzi wa miundombinu ya mawasiliano ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma za intaneti zenye kasi, ubora na uhakika, ambazo zimekuwa mhimili muhimu katika kuendesha shughuli za kijamii na kiuchumi katika dunia ya sasa ya kidijitali.
“Tumekusanyika sio tu kwa ajili ya tukio la uzinduzi, bali kushuhudia hatua inayoongeza kasi ya mageuzi makubwa katika teknolojia ya mawasiliano nchini. Katika safari hii ya mabadiliko, TTCL imeendelea kuwa kinara kwa kuleta ubunifu, kuimarisha miundombinu na kufungua fursa mpya za mawasiliano kwa Watanzania wote,” amesema
Ameongeza kuwa katika enzi ya sasa ya teknolojia ya kidijitali, huduma za intaneti zenye kasi kubwa zimekuwa nguzo muhimu katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, elimu, afya pamoja na ubunifu wa vijana.
“Leo hii dunia inabadilika kwa kasi kubwa. Intaneti yenye kasi, gharama nafuu na uhakika si anasa tena bali ni hitaji la msingi kwa maendeleo ya taifa. Ndiyo maana TTCL imeendelea kuweka nguvu kubwa katika kuboresha miundombinu ya mawasiliano na kupanua huduma ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi,” amesema
Hata hivyo Mwita amesema kuuwa huduma hiyo mpya ya Faiba Supersonic Experience imeboreshwa ili kukidhi mahitaji ya sasa ya wateja wanaotumia teknolojia katika shughuli mbalimbali kama kujenga Smart Home, kuendesha Smart Office, kufanya biashara mtandaoni, kucheza michezo ya mtandaoni pamoja na ku-stream video na maudhui mbalimbali ya kidijitali.
“Huduma hizi zote zinahitaji intaneti yenye kasi kubwa na uhakika. Ndiyo maana TTCL imekuja na huduma hii mpya yenye vifurushi vya kasi ya ajabu ambavyo vitamuwezesha mteja kufanya shughuli zake za kidijitali bila usumbufu wowote,” amesema
Amebainisha kuwa kupitia vifurushi vipya vya Faiba Supersonic Experience, wateja wataweza kuchagua huduma kulingana na mahitaji yao, ikiwemo kifurushi cha T-Fiber Busta chenye kasi ya 60/60 Mbps kwa gharama ya Sh. 55,000 kwa mwezi pamoja na dakika 250 za simu ya mezani.
“Vifurushi vingine ni pamoja na T-Fiber Triple Hub Plus chenye kasi ya 100/100 Mbps kwa Sh. 70,000 kwa mwezi, T-Fiber Triple Hub Extra chenye kasi ya 150/150 Mbps kwa Sh. 100,000 kwa mwezi, T-Fiber Triple Hub Balaa chenye kasi ya 200/200 Mbps kwa Sh. 150,000 kwa mwezi pamoja na T-Fiber Triple Hub Jumbo chenye kasi ya 250/250 Mbps kwa Sh. 200,000 kwa mwezi,” amesema
Ameongeza kuwa wateja watakaojiunga na vifurushi hivyo pia watapata ofa ya laini za simu za mkononi za TTCL bure kulingana na kifurushi watakachochagua.
Kwa mujibu wake, huduma hizo mpya zitawawezesha wateja ku-stream video za ubora wa juu (HD na 4K) bila kukatika, kucheza michezo ya mtandaoni kwa kasi na uhakika, kupakua na kupakia taarifa kwa haraka pamoja na kutengeneza na kusambaza maudhui ya kidijitali kwa ufanisi mkubwa.
Aidha amesema kuwa TTCL itaendelea kuboresha huduma zake ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya wateja katika kipindi hiki cha mapinduzi ya kidijitali.
“Safari ya maboresho ya huduma zetu ndiyo imeanza, na bado tunaendelea kuja na ubunifu zaidi ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora zaidi za mawasiliano. Sasa ni wakati wa kufurahia intaneti ya kweli ya kasi kubwa mlangoni kwako,” amesema




