NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
MAGONJWA yasiyoambukiza yameendelea kuwa tishio kubwa kwa afya ya Watanzania kutokana na kuongezeka kwa wagonjwa na vifo vinavyosababishwa na magonjwa hayo, huku Serikali ikisema imeweka mikakati mipya ya kukabiliana na changamoto hiyo kupitia uimarishaji wa huduma za afya, uchunguzi wa mapema na kinga.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa wakati akifungua Mkutano wa Tatu wa Kimataifa wa Mkakati wa Kikanda wa PEN-Plus (ICPPA 2026) unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo unalenga kujadili utekelezaji wa mkakati wa PEN-Plus katika kuongeza huduma za magonjwa yasiyoambukiza Afrika.
Mchengerwa, amesema Tanzania imeona ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukiza katika kipindi cha miongo minne iliyopita, hali inayohitaji hatua za pamoja kutoka kwa Serikali, wadau na jamii.
Amesema vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza nchini vimeongezeka kutoka chini ya asilimia 25 katika miaka ya 1980 hadi kufikia asilimia 39 mwaka 2021, jambo linaloonesha ukubwa wa changamoto hiyo kwa mfumo wa afya na wananchi kwa ujumla.
Mchengerwa amesema magonjwa ya moyo na mishipa ya damu nayo yameongezeka kwa kasi, ambapo awali yalikuwa yanaathiri chini ya asilimia 5 ya wananchi katika miaka ya 1980 lakini sasa yanaathiri takribani asilimia 20 ya Watanzania.
Amesema saratani imeendelea kuwa miongoni mwa magonjwa yanayochangia vifo vingi nchini, ambapo takribani watu 45,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na ugonjwa huo, huku wanawake wengi wakiathirika zaidi na saratani ya mlango wa kizazi na matiti.
Aidha, Waziri amesema ugonjwa wa seli mundu unaendelea kuchukua maisha ya watoto wengi kabla ya kufikisha umri wa miaka mitano, huku kisukari aina ya kwanza ukiendelea kuathiri watoto na vijana, hali inayohitaji kuimarishwa kwa huduma za uchunguzi na matibabu katika ngazi zote za afya.
Amesema changamoto ya magonjwa yasiyoambukiza haiishii kwenye hospitali pekee bali imekuwa mzigo mkubwa kwa familia, uchumi na jamii kwa ujumla kutokana na gharama za matibabu na ufuatiliaji wa wagonjwa kwa muda mrefu.
“Familia zinapokosa huduma kwa wakati hupoteza siyo tu afya, bali pia muda, kipato na wakati mwingine maisha ya wapendwa wao,” amesema Mchengerwa.
Amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuboresha sera, mikakati na matumizi ya teknolojia katika sekta ya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora karibu na maeneo wanayoishi.
Ameeleza kuwa Tanzania imewekeza katika huduma za afya ya msingi ambapo asilimia 80 ya wananchi sasa wanaweza kupata huduma ndani ya umbali wa kilomita tano kutoka maeneo yao ya makazi, akisisitiza kuwa umbali haupaswi kuwa kikwazo cha mwananchi kupata matibabu.
Mchengerwa amesema Serikali imeongeza vifaa vya uchunguzi na matibabu katika vituo vya afya ikiwemo mashine 700 za X-ray za kidijitali, mashine 1,000 za ultrasound pamoja na vifaa vya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali kama seli mundu, ugonjwa wa moyo na kisukari aina ya kwanza.
Amesema pia hospitali za rufaa zimeongezewa uwezo kupitia uwepo wa mashine 45 za CT Scan, mashine 14 za MRI na mashine moja ya PET CT yenye cyclotron, sambamba na kuongeza mashine za LINAC kutoka tatu hadi nane kwa ajili ya matibabu ya saratani.
Akizungumzia mkakati wa PEN-Plus, Waziri amesema mpango huo ni muhimu katika kusogeza huduma za magonjwa makubwa yasiyoambukiza karibu na wananchi, hasa walioko maeneo ya vijijini na maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa huduma.
Amesema kupitia PEN-Plus, nchi za Afrika zinaendelea kuimarisha huduma za magonjwa kama kisukari aina ya kwanza, ugonjwa wa seli mundu na magonjwa ya moyo katika hospitali za wilaya na vituo vya afya ili kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Profesa Mohamed Janabi, amesema magonjwa yasiyoambukiza kwa sasa yanachangia asilimia 37 ya vifo vyote vinavyotokea barani Afrika, yakiongezeka kutoka asilimia 24 mwaka 2000.
Amesema mkakati wa PEN-Plus ni muhimu katika kukabiliana na changamoto hiyo, kwani unalenga kuboresha huduma za afya kwa wagonjwa wa magonjwa sugu kama kisukari, seli mundu na magonjwa ya moyo, hususan kwa kuhakikisha wanapata huduma karibu bila kusafiri umbali mrefu.
Aidha, amesema mpango huo kwa sasa unatekelezwa katika nchi 20 na umesaidia kuokoa maisha ya zaidi ya watu laki moja, huku nchi kama Rwanda, Malawi na Ghana zikionyesha mafanikio makubwa katika utekelezaji wake.
Profesa Janabi amesisitiza kuwa PEN-Plus si mradi wa majaribio bali ni ushahidi kuwa usawa wa upatikanaji wa huduma za afya barani Afrika unawezekana.

