NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imetangaza maandalizi kabambe ya Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) maarufu Sabasaba, yatakayokwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, huku ikiahidi kuwa maonesho ya mwaka huu yatakuwa makubwa zaidi kuwahi kufanyika.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya maonesho hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Dk. Latifa Mohamed Khamis amesema maonesho ya mwaka huu yatakuwa ya kipekee kutokana na kuadhimisha Jubilee ya Dhahabu ya Sabasaba, hatua inayodhihirisha mchango mkubwa wa maonesho hayo katika kukuza biashara, uwekezaji na uchumi wa Tanzania kwa kipindi cha nusu karne.
Amesema maonesho hayo yataanza rasmi Juni 28 hadi Julai 13, 2026, huku Juni 26 ikitengwa kwa semina maalumu kwa washiriki wote ili kuwajengea uelewa kuhusu huduma mbalimbali zinazopatikana viwanjani na namna ya kunufaika zaidi na ushiriki wao.
“Tunafanya semina hii kwa sababu washiriki wetu wanatoka maeneo mbalimbali, wakiwemo wageni kutoka nje ya nchi. Tunataka wapate taarifa muhimu kuhusu huduma zinazopatikana katika viwanja vya maonesho, ikiwemo usalama, zimamoto, huduma za kijamii na taratibu nyingine muhimu ili waweze kushiriki kwa ufanisi zaidi,” amesema.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, kaulimbiu kuu ya maonesho ya mwaka huu ni “Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba ni Fahari ya Tanzania”, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 50 ya mafanikio ya maonesho hayo.
Amesema pia zipo kaulimbiu ndogo zinazolenga kuhamasisha maendeleo ya biashara na uchumi, ikiwemo “Bidhaa za Tanzania Kimataifa Zaidi” na “Biashara za Tanzania Kidijitali Zaidi”, ambazo zinaakisi dhamira ya Serikali ya kuhimiza matumizi ya teknolojia na kupanua masoko ya bidhaa za Tanzania duniani.
Aidha, amesema kaulimbiu ya hamasa ya mwaka huu ni “Sabasaba 2026 ni Kubwa Kuliko”, akieleza kuwa maandalizi yanayoendelea yanaonesha wazi kuwa maonesho hayo yatakuwa ya aina yake na yenye ushiriki mkubwa zaidi wa wadau wa biashara kutoka ndani na nje ya nchi.
Amesema katika kuelekea kilele cha maadhimisho hayo, TanTrade imeandaa shughuli mbalimbali ikiwemo Walkathon itakayofanyika Juni 27 katika Viwanja vya Mfarasi, ambapo wananchi, wafanyabiashara, viongozi wa serikali na wadau wengine watashiriki matembezi hayo maalumu ya kuhamasisha maonesho ya Golden Jubilee.
Mkurugenzi huyo amesema usiku wa Juni 27 pia kutakuwa na onyesho kubwa la fataki katika Viwanja vya Sabasaba kuashiria kuingia rasmi katika maadhimisho ya miaka 50 ya maonesho hayo.
“Tunataka Watanzania washerehekee nasi mafanikio ya miaka 50 ya Sabasaba. Hii ni historia kubwa kwa taifa letu na ndiyo maana tumeandaa matukio mbalimbali yatakayowapa wananchi burudani na fursa za kujifunza kuhusu biashara,” amesema.
Amesema kama ilivyo desturi, kutakuwa na siku maalumu za nchi mbalimbali (National Days), siku za wafanyabiashara na taasisi za kifedha, huku Julai 30 ikipewa nafasi maalumu na Equity Bank kuwakutanisha wafanyabiashara na wadau wa sekta ya fedha ili kujadili fursa za biashara na uwekezaji.
Dk. Khamis amesema kuwa lengo kuu la maonesho hayo ni kuwakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na wenzao kutoka mataifa mbalimbali ili kuongeza fursa za masoko, uwekezaji na ushirikiano wa kibiashara.
Katika kile kinachotarajiwa kuwa kivutio kikubwa cha maadhimisho hayo, TanTrade imeandaa Usiku Maalumu wa Golden Jubilee utakaofanyika Julai 6, ambapo kutakuwa na maonesho ya kumbukumbu za historia ya Sabasaba, filamu maalumu ya miaka 50, burudani, utoaji wa tuzo na kutambua wadau waliochangia mafanikio ya maonesho hayo kwa kipindi chote cha nusu karne.
“Usiku huo utakuwa wa kipekee sana. Tumewaandalia wadau wetu mambo mengi mazuri yakiwemo simulizi za historia ya Sabasaba, mchango wa viongozi mbalimbali na kutambua watu na taasisi zilizoshiriki kuijenga Sabasaba hadi kufikia mafanikio ya leo,” amesema.

