NA MWANDISHI WETU,DJIBOUTI
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Thabit Kombo amewasili jijini Djibouti, Jamhuri ya Djibouti kwaajili ya kumuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan kwenye sherehe za Uapisho wa Rais Mteule wa nchi hiyo Ismaïl Omar Guelleh.
Kombo amewasili jijini hapo Mei, 08, 2026 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Djibouti-Ambouli na kupokelewa na Waziri wa Bajeti wa nchi hiyo Isman Ibrahim Robleh.
Waziri Kombo anatarajiwa kushiriki katika sherehe hizo za uapisho wa Rais Mteule wa Jamhuri ya Djibouti Mhe. Ismail Omar Guelleh zinazotarajiwa kufanyika jijini hapo leo Mei 09, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Djibouti akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia.
Rais Mteule wa Djibouti Ismaïl Omar Guelleh amechaguliwa kuongoza nchi hiyo kwa muhula wa sita mfululizo kufuatia ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Aprili 10, 2026 nchini humo.




