NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
KIJANA Emmanuel Bombo ametengeneza mashine maalumu kwa ajili ya kuuza mtandao kwa bei rahisi ya Sh.200 hadi 500 ili kuweza kuwafikia watanzania wengi zaidi wenye kipato cha kawaida.
Akizungumza na Demokrasia Digital akiwa ndani ya banda la Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO)katika Maonesho ya 48 ya Biashara Kimataifa yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Bombo alisema kwenye hiyo mashine mtu akitumbukiza kiasi cha Sh. 500 anaweza kupata huduma ya mtandaoni kwa saa 24 huku atakayetumbukiza Sh. 200 atapata huduma hiyo ndani ya saa tano.
Amesema mashine hiyo inayoa huduma ya mtandao kwa bei nafuu kiasi kwamba mtanzania yeyote anaweza kutumia na kupata hduma hiyo.
“Kitu kilichonifanya nivumbue hii mashine niliona watanzania wengi wanatumia muda mwingi kwenye mtandao na wengi wanalalamika kuwa bando haziwatoshi huku zingine ni gharama wanashindwa kumudu.
“Nimeunda hichi kitu ambacho kinaweza kuwapatia huduma hiyo kwa bei nafuu mtu ukiwa n ash. 500 au 200 unaweza kupata huduma ya mtandao na ukaperuzi kitu chochote kile kadiri unavyoweza,” amesema Bombo
Amesema mashine hiyo ina uwezo wa kutoa hudua hiyo ndani ya mita 300 hivyo inaweza kukaa sokoni, au sehemu yoyote ile yenye mkusangiko wa watu wengi.
“Kwa kipindi cha miezi sita tangu nitengeneze mashine hii nimeweza kuwafikia watu zaidi ya 1000 na tumeshaweka kwenye vituo mbalimbali,” amesema
Aidha amesema alifikiria kubuni mashine hiyo baada ya kumaliza elimu yake ya chuo mwaka 2019.