NA MWANDISHI WETU, MTWARA
BENKI ya NMB Kanda ya Kusini imezindua kampeni maalumu kwa wakulima wa kanda hiyo ijulikanayo kama ‘Bonge la Mpango mchongo wa kilimo.
Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kusini, Faraja Ng’ingo alisema kuwa benki hiyo imekuja na kampeni hiyo ili kuendelea kuhamasisha matumizi ya huduma za benki kwa wakulima na vyama vya msingi.
Alisema NMB inatambua na kuuthamini mchango mkubwa wa biashara ya kilimo kwa kanda ya kusini hususani kilimo cha korosho katika ustawi wa benki hiyo na kanda ya kusini hususani mikoa ya Lindi na Mtwara.
Akizungumzia kampeni hiyo alisema mkulima wa korosho sasa akipokea fedha za mauzo kupitia Benki ya NMB mbali ya huduma bora anaweza kuwa miongoni mwa washindi mbalimbali wa zawadi ambazo benki ya NMB imetenga kwa ajili ya kampeni hii.
NMB imetenga pikipiki tano kwa ajili ya wakulima ambapo kila mwisho wa wiki kutaendeshwa droo ya kutafuta mshindi atakaejinyakulia pikipiki hiyo. Droo hii itaendeshwa kwa kipindi cha wiki tano. Pia wakulima wengine watano watajinyakulia fedha taslimu kiasi cha Sh.100,000 kila mmoja katika kila droo.
Ili mtu ashinde zawadi hizo anatakiwa kuwa na akaunti ya Benki ya NMB, ajishughuishe na biashara katika mnyororo wa thamani ya Kilimo na apitishe mauzo yake katika Benki ya NMB.
Aidha katika uzinduzi wa kampeni hiyo droo ya kwanza ilichezeshwa ambapo Mkulima kutoka Newala, Said Likumbeya alijishindia pikipiki.
Akizungumza katika tukio hilo, Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abass aliipongeza Benki ya NMB kwa kuendeleza kampeni hii ya kuhamasisha wakulima kutumia Benki katika kupokea malipo ya mauzo ya mazao yao.
Alisema wakulima wengi wamekuwa wakikutana na maswahibu mbalimbali katika kipindi hiki hasa yanayo husiana na uhalifu sababu ya kukaa na fedha nyingi ndani mwao badala ya kuzihifadhi sehemu salama kama Benki ya NMB.
Aidha Kanali Abbas aliwataka wakulima wa mkoa wa Mtwara kuendelea kuweka akiba ya kutosha ili zawadi nazo zije Mtwara.
Akizungumza katika tukio hio, Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Mwanahamisi Munkunda aliishukuru Benki ya NMB kwa kuendelea kuufungua mkoa wa Mtwara.
