



NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Reli Tanzania ( TRC) limesema kuwa kichwa kipya cha treni ya umeme chenye namba ya usajili E6800-01 kilichoundwa na kampuni ya ‘Hyundai Rotem Company’(HRC) kimewasili nchini Tanzania kutoka nchini Korea Kusini.
TRC iliagiza vichwa vipya 17 vya umeme kutoka ‘Hyundai Rotem Company’ (HRC) ya nchini Korea Kusini vyenye namba ya usajili E6800-01 hadi E6800-17 kwa ajili ya reli ya kiwango cha kimataifa – SGR.
Mfumo wa uendeshaji unaotumika katika kichwa ni nishati ya umeme wenye msongo wa kilovoti 25 na kitakuwa na nguvu ya kilowati 5,000 sawa na nguvu ya 6,800 kwa
kipimo cha ‘Horse Power’.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano cha TRC Jamila Mbarouk , Kichwa kitakuwa na uwezo wa mwendokasi wa kilomita 160 kwa saa (160km/h), kuvuta na kulisha umeme kwenye mabehewa yasiyozidi 14 ya abiria kwa wakati mmoja.
“TRC inatarajia kufanya majaribio ya kichwa cha treni kitakachotumika katika reli ya kiwango cha kimataifa kati ya Dar es Salaam na Morogoro na baadaye Dar es Salaam hadi Dodoma, baada ya kukamilisha ukaguzi wa kichwa na mafunzo ya uendeshaji kwa madereva mapema Disemba 2023. ” ilieleza taarifa hiyo
Aidha taarifa hiyo ilibainisha kuwa, Disemba 2023 TRC inatarajia kupokea vichwa vingine vitatu (3), mpango wa uletaji vitendea kazi utakuwa ukitekelezwa kwa awamu pindi uundwaji wa vitendea kazi unapokamilika.
Vilevile TRC imeshapokea mabehewa 35 kwa ajili ya uendeshaji wa huduma katika reli ya kiwango cha kimataifa.
Kufikia Septemba 2023 mradi wa SGR Dar es Salaam – Morogoro umefikia asilimia 98.6, Morogoro –
Makutupora umefikia asilimia 95.41, Makutupora – Tabora umefikia asilimia 12.32, Tabora – Isaka umefikia asilimia
5.02 na Mwanza – Isaka umefikia asilimia 41.95, Mkandarasi kampuni ya CCECC yuko eneo la mradi kdwa ajili ya maandalizi ya kuanza utekelezaji wa mradi wa SGR awamu ya pili Tabora – Kigoma.