NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imefanikiwa kukusanya tani 27.5 za dhahabu zenye thamani ya takribani Sh. Trilioni 10 kupitia mpango wa kununua dhahabu ulioanzishwa mwaka 2024, hatua inayotajwa kuwa moja ya mafanikio makubwa katika kuimarisha akiba ya fedha za kigeni na uthabiti wa uchumi wa taifa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo katika maadhimisho ya miaka 60 ya Benki hiyo, Gavana wa BoT Emmanuel Tutuba amesema mpango huo umeiwezesha benki hiyo kununua dhahabu inayozalishwa nchini kwa kutumia Shilingi za Tanzania na hivyo kuongeza akiba ya taifa huku rasilimali za madini zikichangia moja kwa moja katika ustahimilivu wa sekta ya fedha.
Amesema mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na mageuzi yaliyofanyika katika sekta ya madini chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, yakiwemo kuimarishwa kwa usimamizi wa sheria, uwazi na matumizi bora ya fursa zilizopo katika sekta hiyo.
“Mpango huu umeendelea kuwanufaisha wadau wote katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini na kuweka rasilimali zetu kama nguzo ya kimkakati ya kujenga ustahimilivu wa muda mrefu wa sekta ya nje na uthabiti wa sekta ya fedha,” amesema
Gavana Tutuba amebainisha kuwa kwa sasa akiba ya fedha za kigeni nchini inatosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa zaidi ya miezi 4.8, kiwango ambacho ni juu ya kigezo cha kimataifa na matakwa ya kisheria ya kuwa na akiba inayoweza kuhudumia angalau miezi minne.
Mbali na mafanikio hayo ya dhahabu, Gavana amesema Tanzania imeendelea kushuhudia mafanikio makubwa ya kiuchumi tangu kuanza kwa mageuzi ya sekta ya fedha, ambapo mfumuko wa bei umedhibitiwa kwa kiwango cha wastani wa asilimia 3.5 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, ukiwa ndani ya lengo la kati ya asilimia 3 na 5.
Amesema hali hiyo ni mafanikio makubwa ikilinganishwa na mwaka 1989 ambapo mfumuko wa bei ulifikia asilimia 35.3.
Katika sekta ya benki, Gavana Tutuba amesema idadi ya benki zilizosajiliwa imeongezeka kutoka benki tatu mwaka 1991 hadi kufikia benki 42 kwa sasa, huku viashiria vya uthabiti wa sekta hiyo vikiendelea kukidhi viwango vya kimataifa.
“Aidha, kiwango cha mikopo chechefu kimeendelea kushuka na kufikia asilimia 2.9 mwezi Februari 2026, chini ya kiwango cha asilimia 5 kinachokubalika kimataifa, jambo linaloashiria kuimarika kwa ubora wa mali za benki na mazingira bora ya biashara nchini,” amesema .
Katika kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia duniani, amesema Benki Kuu imeanzisha kitengo maalumu cha Akili Unde (Artificial Intelligence) na kusaini mikataba ya ushirikiano na vyuo vikuu sita nchini ili kuimarisha matumizi ya teknolojia katika uchakataji wa takwimu, uchambuzi na maamuzi ya kisera.
Kwa mujibu wa Tutuba, mafanikio hayo yanaonesha safari ya miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania iliyojengwa juu ya mageuzi, ubunifu na usimamizi madhubuti wa sera za fedha, hatua ambazo zimeifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye mifumo imara ya kifedha barani Afrika.

