NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
SERIKALI ya Belarus imeonesha nia ya kushirikiana na Tanzania kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuimarisha uchukuzi wa mazao ya kilimo, hususan mbogamboga na nafaka kupitia Bandari ya Dar es Salaam.
Uwekezaji wa kisasa katika Bandari za Tanzania unaendelea kuvutia mataifa mbalimbali duniani, huku Bandari ya Bagamoyo na Bandari ya Tanga zikichagizwa kuwa vituo muhimu vya kuhudumia shehena zinazoharibika kwa haraka.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika Aprili 29, 2026 Makao Makuu ya TPA jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje wa Belarus,Maxima Ryzkhenkov amesema nchi yake imejipanga kuimarisha biashara ya uchukuzi wa mazao yatokanayo na kilimo kupitia Bandari za Tanzania.
Akimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Dk. Baraka Mdima asema Mamlaka ina maeneo kadhaa yanayoweza kutumika kwa ajili ya kuendeleza ushirikiano huo.
Dk. Mdima ametolea mfano wa Bandari kama ya Tanga, kwamba TPA imepanga kufanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya kisasa ya kuweza kuhudumia shehena inayoharika haraka.
Naye Balozi wa Jamhuri ya Belarus nchini, Dzmitry Krasouski amesema wakiwa kama nchi isiyo na Bahari, wamevutiwa mno na uwekezaji mkubwa wa miundombinu uliofanywa katika Bandari ya Dar es Salaam.
Bandari ya Dar es Salaam, ambayo ndio bandari mama, imefanyiwa maboresho makubwa kwa kuongezwa na kurefushwa kwa gati 1-7 ili kupokea meli kubwa zaidi (Panamax/Post-Panamax).
Kina cha maji katika magati kimeongezwa kwa uchimbwa hadi kufikia mita 14.5 ili kuruhusu meli kubwa kuingia bila vikwazo, huku uwezo wa kupokea meli nyingi kwa wakati mmoja ukiongezeka.
Katika bandari hiyo pia, Serikali kupitia TPA kwa kushirikiana na waendeshaji, imewezesha kuongezwa kwa mitambo ya kisasa (RTG cranes, ship-to-shore cranes), kuongezwa eneo la kuhifadhi makontena.
Na kuongezeka kwa kasi ya kushusha na kupakia mizigo kupitia matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA ya kusimamia mizigo (cargo tracking & clearance) pamoja na kupunguza muda wa kushughulikia mizigo (turnaround time).



