NA FLORAH AMON,DAR ES SALAAM
MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk.Peter Kisenge, amewaomba wananchi kujitokeza kuchangia matibabu ya watoto wanaozaliwa na matatizo ya moyo ili waweze kupata huduma hizo bila malipo, pamoja na kusaidia ujenzi wa nyumba za kulala walezi wanaosubiri watoto wao kufanyiwa upasuaji.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Novemba 25, 2026, wakati wa ziara ya mfanyabiashara na Mkurugenzi wa Kampuni ya Kitambaa Cheupe Investment, Jessica Kikumbi, Dk. Kisenge amesema matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo yanahitaji gharama kuanzia Sh milioni 10, ambapo Serikali hugharamia asilimia 70 ya gharama hizo.
Amesema pamoja na Serikali kugharamia sehemu kubwa ya matibabu hayo, asilimia 30 inayobaki bado ni mzigo kwa wazazi wengi, hivyo kuna umuhimu wa wadau na wananchi wengine kujitokeza kutoa michango ili kuwasaidia watoto hao kupata matibabu.
Dk.Kisenge amesema watoto wanaozaliwa na matatizo ya moyo wana nafasi kubwa ya kutibiwa na kupona endapo watawahishwa hospitalini na kupata huduma za kitabibu kwa wakati.
Amesema mbali na kusaidia gharama za matibabu, michango ya wananchi na wadau pia itasaidia kujenga nyumba za kulala walezi ambao hulazimika kusubiri watoto wao wanapokuwa hospitalini wakipatiwa matibabu na kufanyiwa upasuaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitambaa Cheupe Investment, Jessica Kikumbi, amesema kampuni hiyo itatoa sehemu ya mapato itakayopata mwezi Desemba mwaka huu kwa ajili ya kusaidia matibabu ya watoto hao.
Aidha, amewahimiza wananchi na wadau wengine kuweka akiba ya fedha hata kidogo ili kuungana katika juhudi za kusaidia watoto wenye matatizo ya moyo na kuhakikisha wanapata matibabu wanayohitaji.







