NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
IMEELEZWA kuwa matumizi ya virutubisho mbalimbali ( Suppliments) ni kwaajili ya kuimarisha afya na sio kuponya magonjwa sugu kama inavyoelezwa wauzaji wa virubisho hivyo
Aidha virutubisho vilivyopo katika mfumo wa vidonge au unga unga kama vile ‘collagen’ kwaajili ya kuimarisha ngozi vinapaswa kutumika kwa maelekezo ya wataalamu au Daktari sambamba na kuhakikishiwa kuwa vina ubora na viwango stahiki.
Kauli hii imetolewa leo Jumanne Oktoba 27,2026 na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania Dk.Ashura Katunzi katika KikaoKazi baina yake,Ofisi ya Msajili wa Hazina na Wahariri wa Vyombo vya Habari jijini Dar es salaam kueleza mafanikio ya TBS kupitia serikali ya awamu sita
Dk.Katunzi amesema jamii imekuwa ikiaminishwa kuwa Virutubisho hivyo huponya kabisa magonjwa lakini kiuhalisia sivyo ilivyo .
Amesema virutubisho hivyo hutegemeana na mtumiaji anataka kuimarisha afya ya kiungo gani na ndio maana kuna virutubisho kwaajili ya Kucha,ngozi, nywele,mifupa nk.
Ameeleza kuwa hapo ndipo TBS inapoletewa bidhaa kwaajili ya kupima ubora na viwango kwa, kutekeleza jukumu lake ipasavyo mathalani kwenye suala la mifupa itahakikisha bidhaa kweli ina kalsiamu itakayoboresha na kuimarisha afya ya mifupa na sio kinyume chake
” Sasa hivi wanawake wengi tunapenda kung’aa na kuwa na ngozi nzuri kuna virutubisho sahihi ambavyo haviathiri ngozi ,lakini wengi wetu tumekuwa tukitumia bidhaa zisizofaa ambazo zina viambata vyenye sumu na matokeo yake kuishia kupata madhara yanayosababisha kansa ya ngozi…niwaonye wanawake wenzangu” amesisitiza.
Amesema Kwa muktadha huo hapo ndipo TBS huingilia kati na kuondoa kwenye mzunguko vipodozi na virutubisho visivyofaa kwa afya ya binadamu.
Sambamba na hilo Dk Katunzi ametumia fursa hiyo kuwaasa wanawake na wanaume juu ya matumizi ya vipodozi vyenye sumu na kuwataka kuwa mabalozi wazuri wa kutoa taarifa kila wanapotilia Shaka utengenezaji holela wa virutubiaho na vipodozi visivyofaa
Akielezea mafanikio ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) amesema ikumbukwe kwamba lilianzishwa kama sehemu ya jitihada za Serikali katika kuimarisha mustakabali wa sekta za Viwanda na Biashara ili kukuza uchumi wa Taifa na linatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria ya Viwango Sura namba 130.
Ameeleza kuwa Kipindi cha Serikali ya awamu ya Sita (2021-2026), kimekuwa cha mafanikio makubwa kwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika utekelezaji wa majukumu yake. Mafanikio hayo yanaendana na kutimiza azma ya Shirika katika masuala mbalimbali kama ikiwemo kusogeza Huduma Karibu na Wateja
“Katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa ukaribu na kupunguza gharama, Serikali kupitia Shirika la Viwango Tanzania linaendelea na hatua za mwisho za ukamilishaji na makabidhiano ya mradi wa ujenzi wa maabara na ofisi katika eneo la Njedengwa, jijini Dodoma, au kwa jina jingine mradi wa Viwango House – Dodoma wenye thamani ya Sh.Bilioni 24.7 ” amesema Dk.Katunzi
Vilevile Dk.Katunzi ameeleza kuwa Shirika linaendelea na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa ofisi na maabara katika Kanda ya Ziwa eneo la Kiseke Wilaya ya Ilemela Mwanza, mradi unaojulikana kama Viwango House- Mwanza. Mradi huo unakadiriwa kugharimu Sh.Bilioni 12.1
” vilevile Shirika lipo katika hatua za awali za maandalizi za mradi wa ujenzi wa ofisi na maabara Jijini Arusha ( Viwango House -Arusha).Kwa upande wa Dodoma, maabara zilizojengwa zinahudumia pia mikoa ya karibu na Dodoma hususani Singida na Tabora.
” Aidha, maabara za Mwanza zinatarajiwa kuhudumia mikoa sita, ambayo ni Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Shinyanga na Simiyu. Hatua hiyo ya ujenzi wa ofisi na maabara itasaidia kusogeza huduma karibu na wananchi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa majibu ya vipimo vya sampuli
*Serikali kupitia TBS imetumia zaidi ya Sh.Bilioni 9.8 kwa ajili ya kuimarisha ofisi tisa za kanda (Arusha, Mwanza, Mtwara, Dar es Salaam, Dodoma, Kigoma, Mbeya, Pwani na Geita) pamoja na ofisi za mipakani (Tunduma, Kasumulo, Horohoro, Holili, Tarakea, Namanga, Bandari ya Mwanza, Uwanja wa Ndege wa Mwanza, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, Sirari, Kabanga, Rusumo, Mutukula, Kasesya, Bandari ya Bagamoyo, bandari ya Mbweni, bandari ya Dar es Salaam, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere na Bandari ya Tanga) kwa kuongeza ofisi mpya za kanda, wafanyakazi na vitendea kazi kwa ajili ya kutoa huduma kwa wakati na kuimarisha zoezi la ukaguzi wa mara kwa mara katika soko ili kupunguza bidhaa hafifu sokoni na hatimaye kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa bora na salama.”amebainisha Dk.Katunzi
Katika hatua nyingine Dk.Katunzi amesema TBS imefanikiwa kuwezesha Biashara; Ili kuwezesha Biashara, Shirika lina Kamati za Kitaalam (Technical Commitees) za Uandaaji Viwango 117 katika sekta ya chakula, kemikali, uhandisi mitambo, uhandisi umeme, uhandisi ujenzi, nguo na ngozi, madini na mitambo ya uchimbaji madini, mazingira na taaluma mtambuka (general tecniques).
Kadhalika amesema, Katika mchakato wa kuandaa viwango Kamati hizo zinashirikisha wadau mbalimbali ikiwemo vyuo vikuu, taasisi za utafiti, wafanyabiashara, wazalishaji, vyama vya walaji, vyama na bodi za wataalam, taasisi za udhibiti na watunga sera. Katika kipindi cha Serikali ya awamu ya sita Shirika limefanikiwa kuandaa viwango 3901 vya sekta mbalimbali kwa kuzingatia mahitaji ya soko ambavyo vinasaidia wafanyabiashara, wajasiriamali na watoa huduma kuzalisha bidhaa bora zenye kukidhi matakwa ya viwango, hivyo kuwawezesha kufanya biashara ndani na nje ya nchi, hatua ambayo italeta tija na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Aidha, jumla ya vyeti na leseni za ubora 3,940 vimetolewa kwa wazalishaji, miongoni mwao wakiwemo wajasiriamali wadogo 1,683. Serikali kupitia TBS imekuwa ikitenga zaidi ya Sh. Milioni 300 kila mwaka kwa madhumuni ya kuhudumia wajasiriamali wadogo bila ya malipo yoyote. Leseni hizi zimesaidia wazalishaji kuweza kuzalisha bidhaa bora, ikiwa ni pamoja na bidhaa zao kuweza kuaminika sokoni na pia kufanya biashara nje ya mipaka ya Tanzania, hivyo kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa
“Shirika limeendelea na huduma za usajili wa bidhaa za chakula na vipodozi pamoja na maeneo ya uzalishaji, uuzaji, usambazaji na uhifadhi wa chakula na vipodozi kwa lengo la kuhakiki ubora na usalama wa maeneo hayo ili kuendelea kulinda afya za walaji ambapo jumla ya bidhaa 9,731 zilisajiliwa na maeneo 80,836 yalisajiliwa.
” Pia, katika kuimarisha ukaguzi wa bidhaa mbalimbali zinazoingia nchini kutoka nchi za nje, TBS huhakiki ubora wa bidhaa na magari yaliyotumika kabla ya kusafirishwa kuja nchini ambapo katika kipindi cha serikali ya awamu ya sita jumla ya shehena za bidhaa 183,186 zilikaguliwa kabla ya kuingia nchini kupitia mfumo wa Pre-Shipment to Conformity (PVoC) na shehena za bidhaa 426,842 zilikaguliwa baada ya kufika nchini kupitia mfumo wa Destination Inspection (DI).
” Jumla ya magari 249,386 yalikaguliwa. Bidhaa hizi zinakaguliwa kwa lengo la kuiepusha Tanzania kuwa jalala la bidhaa duni pamoja na kulinda afya, usalama na mazingira ya watumiaji.Kwa upande wa mafunzo, TBS imeweza kutoa mafunzo kwa jumla ya wadau 6824 wakiwemo wazalishaji wa bidhaa za viwandani na wasindikaji.
” Mafunzo hayo yalihusu dhana nzima ya viwango na ubora ambayo yatawawezesha kuzalisha bidhaa zinazokidhi matakwa ya viwango na yamewawezesha kupata uelewa mpana kwenye masuala ya udhibiti ubora, hivyo kuwaandaa kuhimili ushindani wa masoko ya ndani, kikanda na kimataifa”amesema
Wakati huo huo Dk.Katunzi amejinasibu kuwa , TBS imeendelea kutoa elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali ili kukuza uelewa juu ya masuala ya viwango na udhibiti ubora. Njia hizo ni pamoja na kuanzisha kliniki ya Viwango ambayo inaendelea katika maeneo mbalimbali; pamoja na kushiriki katika makongamano, maonesho, warsha na semina; kuandaa mikutano na wadau wa masuala ya viwango, kutoa mafunzo mbalimbali kuhusu masuala ya ubora na usalama; na kuendesha kampeni za elimu kwa umma katika ngazi za wilaya. Aidha, elimu imekuwa ikitolewa kupitia vyombo vya habari zikiwemo redio jamii, redio za kitaifa, runinga, magazeti, mitandao ya kijamii, matangazo, majarida na vipeperushi.
Pia Dk. Katunzi amesema mafanikio mengine ni kuongeza Ufanisi wa Maabara; TBS ina jumla ya maabara 14 na zote zimeweza kupata ithibati za umahiri, ambapo maabara hizo zimehakikiwa na kupatiwa vyeti vya ithibati ya umahiri wa kimataifa. Hatua hiyo inamaanisha kuwa majibu ya sampuli kutoka katika maabara hizo yanaaminika na kukubalika popote duniani na hivyo kurahisisha biashara ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu. Katika kipindi hicho TBS imeweza kupima sampuli zaidi ya 188,952 na kufanyia ugezi vifaa 54,396 ambapo suala hili litasaidia kuhakikisha katika soko kunakuwa na bidhaa zenye ubora.Pia, maabara hizo zina mashine za kisasa (state-of -art-equipment) zinazopelekea kupata majibu kwa wakati na sahihi, Serikali imeweza kutumia kiasi kisichopungua Sh. Bilioni 12.9 kuhakikisha mashine hizi zinapatikana.
” Pamoja na mashine nyingi zilizopo katika maabara hizo, kuna mashine za kipekee kama ifuatavyo;Mashine ya hydrostatic pressure test ya kupima mabomba ya maji na yenye uwezo wa kupima mabomba yenye kipenyo cha milimita 12 sawa na inch 0.5 hadi milimita 800 sawa na inchi 32. Mashine hii ina uwezo pia wa kupima sampuli 120 kwa wakati mmoja na kati ya nchi 54 za Barani Afrika inapatikana katika nchi tano tu ikiwemo Tanzania;Mashine ya automatic conductor resistance tester ya kupimia waya (cables) za umeme za aina zote zenye kipenyo hadi kufikia milimita 40 sawa na milimita za mraba 1200. Mashine hii ni ya kipekee kwa kuwa ni ya kidigitali na ina uwezo wa kupima na kutoa majibu kwa haraka; Mashine ya solar simulator ambayo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati inapatikana Tanzania pekee katika ofisi zetu za TBS
“Mashine hii inauwezo wa kupima solar panels za aina zote bila kutegemea uwepo wa jua. Ndugu Wanahabari,Jambo la nne ni, Kuimarisha Mifumo ya TEHAMA- ICTM Shirika linatumia mifumo ya TEHAMA katika utoaji wa huduma zake mbalimbali kama vile leseni ya ubora, ukaguzi wa shehena zinazotoka nje ya nchi na usajili wa bidhaa za chakula na vipodozi, majengo, maeneo ya uzalishaji, uuzaji, vyombo vya usambazaji wa bidhaa za chakula na vipodozi. Mifumo hiyo ni OAS na i-SQMT. Aidha, Shirika limeboresha huduma zake kwa wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa nchini kwa kuunganisha mfumo wake unaoitwa Online Application System na mfumo wa Dirisha Moja la Huduma (Tanzania electronic Single Window System – TeSWS) ambapo mfanyabiashara anatuma maombi na anapata huduma za taasisi zote kupitia mfumo huo”
Pamoja na mambo mengine Dk .Katunzi ameonesha kuridhishwa na TBS kuanza utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya KupikiaSerikali katika kuboresha upatikanaji wa nishati safi, kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, na kutunza mazingira huku ikiokoa maisha kupitia suluhisho endelevu la upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kupitia TBS na washirika wa maendeleo na Wizara ya Nishati imeanza kuandaa viwango vya ufanisi wa nishati kwa vifaa vya umeme vya majumbani.
“Vifaa vya Maabara vya kisasa vinaendelea kununuliwa kwa ajili ya kuhakikisha vifaa vinavyoingia sokoni vinakidhi viwango vilivyowekwa kabla ya kuwafikia watumiaji. Hatua hii inalenga kupunguza uzalishaji wa gesi ya ukaa na hivyo kulinda mazingira, na pia kupunguza upotevu wa nishati, na hivyo kupunguza gharama kwa watumiaji
“Mafanikio hayo yote, yamepelekea Shirika Kupokea Tuzo na tambuzi kadhaa za hadhi ya juu kutokana na utendaji wake bora wa usimamizi wa viwango na mchango wake katika kuhakikisha ubora, usalama wa umma, na ubunifu katika utoaji wa huduma kwa umma katika kipindi husika kama ifuatavyo:Utambuzi huu unaakisi juhudi za pamoja za Wizara ya Viwanda na Biashara, Bodi, Uongozi na wafanyakazi wote wa TBS katika kuhakikisha kuwa bidhaa zilizopo sokoni zinakidhi viwango vinavyohitajika na ni salama kwa walaji. Hii inaimarisha sifa ya TBS kitaifa, kikanda na kimataifa, na kufungua fursa za ushirikiano zaidi na washirika wa kimataifa”amesisitiza Dk.Katunzi
,Akihutimisha kuekeza mafanikio ya Shirika hilo Mkurugenzi huyo ametanabaisha kuwa Serikali kupitia TBS inaendelea na juhudi za kuweka na kutekeleza mikakati mbalimbali ili kuboresha huduma kwa lengo la kuwezesha biashara kwa madhumuni ya kuinua uchumi wa viwanda kwa kuchagiza uzalishaji wa bidhaa salama na bora hapa nchini kama njia mojawapo ya kuchangia pato la Taifa lakini pia ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi imara wa Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake na kuendelea kuisimamia na kuwa TBS hii inayoonejana iking’ara kitaifa na kimataifa.





