NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
WAKATI magonjwa yasiyoambukiza yakizidi kuwa tishio kwa afya na uchumi duniani, Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) kimeiomba Serikali kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kutunga kanuni ya lazima ya kudhibiti matumizi ya Trans Fatty Acids (TFA) kwenye vyakula, ikisema hatua hiyo itaokoa maisha ya maelfu ya Watanzania na kuifanya nchi kufikia viwango vya kimataifa vya usalama wa chakula.
Trans Fatty Acids, maarufu kama Trans Fat, ni aina ya mafuta yasiyo na afya ambayo kwa kiasi kikubwa hutengenezwa viwandani kupitia mchakato wa kubadili mafuta ya mimea kuwa magumu au nusu magumu (Partially Hydrogenated Oils – PHO).
Mafuta hayo hutumika kuongeza muda wa kuhifadhi bidhaa za chakula, kuboresha ladha na muundo wake, na hupatikana kwenye baadhi ya bidhaa kama biskuti, keki, maandazi, vyakula vya kukaanga na vyakula vya haraka (fast foods).
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), matumizi ya Trans Fats Acids husababisha zaidi ya vifo 278,000 kila mwaka duniani, huku yakichangia ongezeko la magonjwa ya moyo na mishipa ya damu. WHO pia imeeleza kuwa ulaji wa Trans Fat huongeza hatari ya kupata ugonjwa wa moyo kwa asilimia 21 na huongeza hatari ya vifo vinavyotokana na ugonjwa huo kwa asilimia 28.
Licha ya WHO kuweka lengo la kuondoa mafuta hayo kwenye mfumo wa chakula duniani ifikapo mwaka 2023 kupitia mpango wa REPLACE, bado nchi nyingi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania, hazijawa na kanuni za lazima zinazodhibiti matumizi yake.
Akizungumza jijini Dar es Salaam na Mwandishi wa Makala haya Mkurugenzi Mtendaji wa TAWLA, Tike Mwambipile anasema ni wakati sasa Tanzania kuchukua hatua za kisheria ili kulinda afya za wananchi.
Anasema TAWLA inapendekeza kanuni itakayotungwa na TBS izingatie masharti mawili muhimu yanayopendekezwa na WHO. “Kwanza, iweke kiwango cha juu cha Trans Fatty Acids kisichozidi gramu mbili kwa kila gramu 100 za mafuta yote yaliyomo kwenye chakula, sawa na asilimia mbili. Pili, ipige marufuku matumizi ya Partially Hydrogenated Oils (PHO) ambazo ndizo chanzo kikuu cha Trans Fat zinazozalishwa viwandani,” anasema.
Anaeleza kuwa hatua hiyo itawezesha kupunguza mzigo wa magonjwa yasiyoambukiza kama vile magonjwa ya moyo, kiharusi na kisukari, ambayo yanaendelea kuongezeka nchini.
“Hatua hii itasaidia kulinda afya za wananchi, kupunguza magonjwa ya moyo na mengine yasiyoambukiza, pamoja na kuiwezesha Tanzania kuendana na viwango vya kimataifa vya usalama wa chakula,” amesema.
Kwa mujibu wa WHO, magonjwa yasiyoambukiza huchangia takribani asilimia 74 ya vifo vyote duniani, huku magonjwa ya moyo na mishipa yakisababisha zaidi ya vifo milioni 17.9 kila mwaka, idadi kubwa kuliko ugonjwa mwingine wowote.
Tike anasema afya bora ni msingi wa haki na maendeleo ya jamii, ndiyo maana TAWLA inaona sheria kama nyenzo muhimu ya kuzuia madhara kabla hayajatokea.
“Hatuwezi kuwa na jamii yenye usawa na haki kama hakuna afya bora. TAWLA tunatumia sheria, hasa kwa kuangalia mfumo wa kijinsia, kama nyenzo ya kuzuia madhara kabla hayajatokea,” anasema.
Kwa upande wake, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Chuo Kikuu cha Cape Town (UCT), Afrika Kusini, Profesa Frederick Mashili, anasema Serikali inapaswa kuharakisha uwekaji wa sera na viwango vya kitaifa vya kudhibiti Trans Fat.
Anasema mafuta hayo yanachangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza ambayo yanaathiri uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla kutokana na gharama kubwa za matibabu na kupungua kwa uzalishaji.
“WHO ilijiwekea lengo kwamba ifikapo mwaka 2023 dunia nzima iwe imeweka sera za kudhibiti Trans Fatty Acids. Kinachosikitisha ni kwamba nchi zilizoendelea tayari zimefanya hivyo na zimepiga hatua kubwa, wakati nchi nyingi zinazoendelea bado hazijachukua hatua,” anasema
Profesa Mashili anasema tafiti zilizofanyika tayari zimethibitisha madhara ya Trans Fat, hivyo hakuna sababu ya kuchelewa kutunga sera na kanuni.
“Tafiti zimetoa ushahidi wa kutosha. Kilichobaki sasa ni kuzitafsiri tafiti hizo kuwa sera na kanuni zitakazopunguza tatizo hili nchini,” anasema Profesa Mashili
Kwa upande wake Mtaalamu wa lishe kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Profesa Joyce Kinabo anasema pamoja na kuweka viwango vya Trans Fat, Tanzania inahitaji kuboresha mfumo wa uwekaji wa lebo za lishe (nutrition labelling) kwenye bidhaa za chakula.
Anasema watumiaji wengi hushindwa kufanya uchaguzi sahihi wa bidhaa kutokana na ukosefu wa taarifa wazi kuhusu kiwango cha mafuta, sukari, chumvi na virutubisho vilivyomo kwenye bidhaa.
“Kuboresha mfumo wa lebo kutawasaidia wananchi kuelewa wanachokula na kufanya maamuzi sahihi kuhusu afya zao,” anasema Profesa Kinabo
Aidha, Profesa Kinabo ameiomba TAWLA kuendelea na juhudi zake za kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya Trans Fatty.
“Naiomba TAWLA isiache juhudi hizi. Kadri wananchi watakavyopata elimu, ndivyo watakavyokuwa na uwezo wa kudai bidhaa salama na kufanya uchaguzi bora wa chakula,” anasema Profesa Kinabo
Kwa mujibu wa takwimu za WHO, hadi sasa zaidi ya watu bilioni 3.7 duniani wanalindwa na sera za kudhibiti Trans Fat baada ya nchi zaidi ya 60 kutekeleza kanuni zinazopiga marufuku matumizi ya Partially Hydrogenated Oils (PHO) au kuweka kiwango cha juu cha asilimia mbili ya Trans Fat kwenye mafuta na vyakula.
Wataalamu wanaamini kuwa Tanzania ikifuata hatua hizo, itaokoa maisha ya wananchi wengi, kupunguza gharama za matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza na kuimarisha ubora wa bidhaa zake za chakula katika soko la ndani na la kimataifa.

