NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amewataka wafanyabiashara na watoa huduma nchini kuanza kujiandaa mapema kunufaika na fursa za kiuchumi zitakazotokana na mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, yatakayofanyika kwa pamoja Tanzania, Kenya na Uganda.
Makonda ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam katika hafla ya ufunguzi wa Ofisi za sekretarieti ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) nchini Tanzania.
Amesema mashindano hayo yanatarajiwa kuvutia wageni, timu na mashabiki kutoka mataifa mbalimbali, hivyo kutoa fursa kubwa kwa wafanyabiashara katika sekta za hoteli, usafiri, utalii, usafi, matangazo na biashara ndogo ndogo kuongeza wateja na kipato.
Amesema wafanyabiashara wanapaswa kupanua biashara zao, kuzisajili, kuzitangaza kupitia mitandao ya kijamii na kuimarisha mifumo ya malipo ya kidijitali ili waweze kuhudumia wageni watakaotembelea Tanzania wakati wa mashindano hayo.
Aidha, amewahimiza wananchi kujifunza lugha za kimataifa zikiwemo Kiingereza, Kifaransa na Kiarabu ili kurahisisha mawasiliano na wageni, akisisitiza kuwa maandalizi ya AFCON hayapaswi kuishia kwenye viwanja na miundombinu pekee, bali yanapaswa kuwashirikisha wananchi katika kunufaika na fursa za kiuchumi.
Makonda amesema AFCON 2027 ni tukio la kihistoria kwa Afrika Mashariki, kwa kuwa nchi hizo tatu zitakuwa mwenyeji wa mashindano hayo yatakayochezwa kwa siku 29, yakihusisha timu 24 na jumla ya mechi 52.
Amesema Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa sehemu kubwa ya mechi hizo katika miji ya Dar es Salaam, Arusha na Zanzibar, huku serikali ikiendelea kujiandaa kuhakikisha timu, viongozi, mashabiki na wageni wanapata huduma zinazostahili.
Ameeleza kuwa mafanikio ya mashindano hayo hayapaswi kupimwa kwa ubora wa viwanja, idadi ya mabao au shangwe za mashabiki pekee, bali pia kwa ukuaji wa biashara, ongezeko la watalii na mabadiliko ya maisha ya wananchi yatakayotokana na fursa zitakazopatikana.
Katika hatua nyingine, Makonda amewapongeza viongozi wa Tanzania, Kenya na Uganda, akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan, Rais Yoweri Museveni na Rais William Ruto, kwa kushirikiana kuhakikisha maandalizi ya mashindano hayo yanaendelea.
Amesema Tanzania inapaswa kutumia nafasi hiyo kujitangaza kimataifa, kukuza biashara na utalii pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kikanda, akisisitiza kuwa fursa ya AFCON imekuja na ni wajibu wa wananchi kuitumia kujenga uchumi wao.
Naye Katibu Mkuu wa CAF, Samson Adam ametoa pongezi za dhati kwa serikali ya Tanzania na Bodi ya Utalii nchini(TTB) kwa kuliamini shirikisho hilo na kulipatia mapokezi mazuri.
Adam amesema kuwa Tanzania imekuwa nchi nzuri yenye ukarimu, uzuri wa vivutio na mapokezi mazuri kwa wageni mbalimbali akiwemo yeye.




