NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Afya, Mohamed Mchengerwa amesema Serikali inaendelea kuimarisha huduma za afya nchini kwa kuboresha upatikanaji wa huduma za mama na mtoto pamoja na kusogeza vituo vya kutolea huduma karibu na wananchi.
Amesema hatua hiyo inalenga kupunguza umbali unaotembea wananchi kufuata huduma za afya, hususan wajawazito na watoto wachanga, ili kuhakikisha wanapata huduma kwa wakati na kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa ujauzito na kujifungua.
Mchengerwa ameyasema hayo leo Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio yaliyopatikana kutokana na ziara iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan nchini Ethiopia.
Ameeleza kuwa uwepo wa vituo vya afya karibu na maeneo wanayoishi wananchi ni muhimu katika kuboresha huduma za uzazi na kuongeza uwezekano wa watoto kupata huduma bora za afya tangu wanapozaliwa.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Wizara ya Afya, mifumo ya utoaji huduma na wadau mbalimbali ili kuhakikisha rasilimali zilizopo zinatumika kwa ufanisi katika kuboresha sekta hiyo.
26/11/IMG-20261124-WA0042-300×197.jpg” alt=”” width=”300″ height=”197″ class=”alignnone size-medium wp-image-25592″ />
Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi wote na kuimarisha ustawi wa jamii.
Naye Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Bruno Sunguya amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za afya, mashirika ya kiraia na sekta binafsi ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma za afya na kuimarisha mifumo ya afya nchini.
Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuunganisha mipango na mifumo ya taasisi mbalimbali, kubadilishana uzoefu na maarifa pamoja na kutumia rasilimali zilizopo kwa pamoja katika kukabiliana na changamoto za sekta ya afya.
Ameeleza kuwa taasisi za ndani na nje ya nchi zinapaswa kushirikiana katika utekelezaji wa afua mbalimbali za afya, kufanya tafiti na kuimarisha mifumo ya utoaji huduma ili kuongeza uwezo wa taasisi hizo kufikia malengo yake.
Aidha, Profesa Sunguya amesema ushirikiano huo unapaswa kuzingatia maeneo muhimu ya maendeleo ya jamii, ikiwemo afya ya uzazi, afya ya mama na mtoto pamoja na uwezeshaji wa wanawake na vijana.
Katika hatua nyingine, ameeleza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za afya na mashirika ya kiraia ili kuongeza uhamasishaji wa jamii, kushiriki katika utekelezaji wa programu za afya na kuimarisha huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Amesema mashirika hayo yana nafasi muhimu katika kusaidia utekelezaji wa programu mbalimbali za afya, hasa kwa kuunganisha jamii na taasisi zinazohusika na utoaji wa huduma.
Pia amesisitiza umuhimu wa sekta binafsi kushiriki katika maendeleo ya sekta ya afya, hususan katika uwekezaji wa vifaa tiba, bidhaa za afya, teknolojia na miundombinu ya kutolea huduma.
Amesema ushiriki wa wadau hao utasaidia kuongeza rasilimali, ujuzi na uwezo wa mifumo ya afya nchini.



