NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amewataka wahitimu wa Taasisi ya Uongozi kuwa waadilifu, wenye nidhamu na uthubutu ili kuchangia maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Ridhiwani amesema hayo Mei 15, 2026 wakati wa Mahafali ya Tisa ya Taasisi hiyo yaliyofanyika Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Amesema katika ulimwengu wa sasa, uadilifu ni sifa muhimu kwa kiongozi bora na mwenye kuaminika, huku akiwataka wahitimu kutumia maarifa na ujuzi walioupata kuwa viongozi wanaozingatia haki, uwajibikaji na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Nawakumbusha umuhimu wa kuwa viongozi wenye uzalendo. Tukumbuke msemo wa wahenga: Adhabu ya msaliti ni malipo ya usaliti wake. Usaliti mkubwa katika uongozi wa umma ni sawa na ubadhirifu wa mali za umma,” amesema Ridhiwani.
Aidha, amewasihi Wahitimu hao kuwa viongozi wenye maadili mema, wanaolinda mali za umma na kuweka mbele maslahi ya wananchi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Amesema Taifa linahitaji viongozi waaminifu, wenye uwajibikaji na wanaotumia nafasi zao kusukuma mbele maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa manufaa ya Watanzania wote.
Sambamba na hayo, Ridhiwani amesisitiza kuwa uongozi bora unaozingatia haki na uwazi utaendelea kuitangaza vyema Tanzania pamoja na Taasisi ya Uongozi ndani na nje ya nchi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo ya Uongozi, Kadari Singo amesema katika Mahafali hayo, jumla ya Wahitimu 231 wametunukiwa vyeti na kutambuliwa kwa mafanikio yao baada ya kukamilisha mafunzo katika programu mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo.
Singo amezitaja programu hizo ni pamoja na Postgraduate Diploma in Leadership (PGD), Certificate in Leadership (CiL), Women’s Leadership Programme (WLP) pamoja na Emerging Leaders Programme (ELP) ambazo zinalenga kuwajengea washiriki uwezo wa kiuongozi, usimamizi na kufanya maamuzi yenye tija katika taasisi zao na jamii kwa ujumla.
Amesema washiriki wa programu hizo za mafunzo ya uongozi wameeleza namna zilivyowasaidia kuongeza uwezo na kujiamini katika nafasi zao za uongozi pamoja na kuboresha utendaji kazi katika taasisi wanazozihudumia.
“Wamesema kupitia programu hizo wamepata ujasiri na uwezo mkubwa wa kuongoza, kufanya maamuzi yenye tija na kusimamia vyema majukumu yao ya kila siku. Aidha, mafunzo hayo yamechangia kuboresha sera, mifumo pamoja na taratibu za kazi ndani ya taasisi mbalimbali hali inayosaidia kuongeza ufanisi wa utoaji huduma,” amesema Singo
Akizungumza kwa niaba ya wahitimu, Mkurugenzi Mtendaji Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), Juma Burhan Mohamed amesema mafunzo hayo yamekuwa chachu ya mabadiliko makubwa katika fikra, uwezo wa kuongoza na namna ya kufanya maamuzi yenye tija kwa taasisi na jamii.
Amesema mahafali hayo hayakuwa tu sherehe ya kukamilisha mafunzo, bali ni ishara ya mabadiliko na ukuaji wa kiuongozi walioupata ndani ya kipindi cha miezi sita ya programu hiyo.
Burhan amesisitiza kuwa katika kipindi cha mafunzo hayo, washiriki walijifunza masuala mbalimbali ikiwemo uwezo wa kusikiliza, utoaji wa maamuzi kwa kutumia ushahidi pamoja na kujiongoza binafsi kabla ya kuwaongoza wengine.
Amesema kupitia mafunzo hayo waliyoyapata watawasaidia kuendelea kujenga uaminifu, kuthamini tofauti za watu na kuunda mtandao wa viongozi wenye maono ya pamoja.
“Mafunzo haya yametubadilisha kwa kutufanya kuwa viongozi wenye uwajibikaji zaidi, wanaotambua nguvu tuliyonayo na umuhimu wa kuongoza kwa uadilifu kwa ajili ya maendeleo ya taasisi na bara la Afrika kwa ujumla,” amesema







