NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
WAKALA wa vipimo Mkoa wa Kinondoni (WMA) wametoa rai kwa wananchi kuendelea kutumia vipimo sahihi ili kupata bidhaa zenye viwango husika na si kupunjwa.
Akizungumza jana Mei 19,2026 na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani inayoadhimishwa leo, Meneja wa Wakala hao Mkoa wa Kinondoni, Lilian Mombheki, amesema kuwa kumekuwa na hulka kutoka kwa baadhi ya watu kuendelea kutumia vipimo visivyo halali kwa makusudi ili kujinufaisha wao.
“Suala la kutumia mzani kwa walaji ni muhimu ambapo nchi mbalimbali wamebaini kwamba matumizi ya vipimo hualalisha usawa wa bidhaa kwa mnunuzi na muuzaji ,”amesema Mombheki .
Aidha Mombheki amesema kwamba kwa mwaka huendesha zoezi la uhakiki wa mizani pamoja na utoaji wa elimu katika kutumia vipimo sahihi kwa bidhaa salama kwa watumiaji.
Hata hivyo Wakala hao huwachukulia hatua za kisheria kwa kuwatoza faini wale wote wanaokiuka utaratibu wa kuuza ama kununua bidhaa zisizo na ubora kwa lengo la kuwauzia wengine.
Kilele cha siku ya vipimo duniani kimepambwa na kauli mbili ya mwaka huu isemayo vipimo hujenga Imani katika sera za biashara na uchumi ambapo kila mfanyabiashara lazima awe na Imani na Soko lake katika kumlinda mteja dhidi ya upatikanaji wa bidhaa salama na usahihi wa vipimo.

