NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari Tambaza wameeleza kufurahishwa na ujio wa wataalamu kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) waliotembelea shule hiyo na kutoa elimu kuhusu kozi mbalimbali zinazotolewa chuoni hapo pamoja na namna ya kuomba kujiunga baada ya kuhitimu elimu ya sekondari.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa shule hiyo, Kelvin Mwachahe alisema ujio wa NIT umeongeza uelewa mkubwa kwa wanafunzi kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya usafirishaji na teknolojia.
Alisema wanafunzi wengi hawakuwa na uelewa mpana kuhusu kozi zinazotolewa katika chuo hicho, lakini baada ya kupata elimu wameweza kufahamu masomo mbalimbali yanayotolewa pamoja na kozi zinazopata mikopo kutoka serikalini.
“NIT wamefungua mawazo yetu na kutupa mwanga kuhusu kozi mbalimbali zinazotolewa chuoni hapo pamoja na namna ambavyo tunaweza kujiunga baada ya kuhitimu masomo yetu,” alisema Kelvin.
Kwa upande wake, mwanafunzi wa kidato cha tano, Amina Farasi alisema mafunzo hayo yamemsaidia kufahamu kuwa NIT inatoa kozi nyingi zikiwemo za urubani wa ndege pamoja na uwepo wa mikopo hata kwa wanafunzi wa ngazi ya cheti.
Amesema jambo hilo limempa hamasa kubwa ya kujiunga na chuo hicho mara baada ya kumaliza elimu yake ya sekondari.
“Nilikuwa sijui kama kuna mikopo hata kwa baadhi ya kozi za cheti, lakini sasa nimepata motisha kubwa ya kusoma NIT hasa katika kozi zinazohusiana na urubani,” alisema Amina.
Naye Mkuu wa shule hiyo, Dk. Hussein Mavumba alisema ziara ya NIT imekuwa na manufaa makubwa kwa wanafunzi kutokana na kozi zinazotolewa chuoni hapo kuendana na mahitaji ya sasa ya taifa.
Alisema serikali imeweka mkazo mkubwa katika elimu ya amali na uzalishaji wa wataalamu wengi wa kada mbalimbali ifikapo mwaka 2030 ili kusaidia kukuza uchumi wa nchi.
“Kozi zinazotolewa NIT zinaendana moja kwa moja na dira ya serikali ya kuzalisha wataalamu na wahandisi wengi watakaosaidia maendeleo ya taifa letu,” alisema Dk. Mavumba.
Awali mafunzo Mkufunzi wa Urubani kutoka NIT, Ally Ramadhani alisema kwa sasa chuo hicho kinatoa mafunzo ya awali ya urubani na kwamba mwanafunzi anayehitaji kujiunga anatakiwa kuwa na ufaulu mzuri hasa katika masomo ya hisabati, fizikia, jiografia, Kiingereza na kemia.
Alisema ujio wa ndege mpya za mafunzo utaongeza uwezo wa chuo hicho katika kuandaa marubani wenye uwezo mkubwa wa kuendesha ndege za kisasa.
Kwa upande mwingine, Mkufunzi kutoka NIT, Emmanuel Raphael alisema chuo hicho pia kinaendesha Kituo cha Kikanda cha Usalama Barabarani kilichoanzishwa na serikali mwaka 2020 kwa lengo la kutoa elimu ya usalama barabarani kwa jamii hususan wanafunzi.
Alisema wanafunzi ni miongoni mwa waathirika wakubwa wa ajali za barabarani, hivyo elimu hiyo imelenga kuwajengea uelewa wa namna salama ya kutumia barabara wanapokwenda na kurejea kutoka shuleni.
“Tunataka kuhakikisha kizazi chetu kinakuwa salama ili kiweze kuendelea kupata nafasi ya kulitumikia taifa katika sekta mbalimbali,” alisema Raphael.






