NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
TAASISI ya Uongozi imezindua Mpango Mkakati wake wa nne wa miaka mitano kwa kipindi cha 2026/27 hadi 2030/31, ukiwa na lengo la kuendeleza uongozi kwa maendeleo endelevu barani Afrika.
Mpango huo mpya umeelezwa kuwa ni mwendelezo wa mafanikio yaliyopatikana katika mipango mitatu iliyopita, huku ukiweka vipaumbele vipya vinavyolenga kukabiliana na changamoto zinazoibuka kitaifa, kikanda na kimataifa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika wakati wa mahafali ya tisa ya Taasisi ya Uongozi, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa taasisi hiyo, Ombeni Sefue amesema mkakati huo unalenga kuanzisha programu bunifu za kimkakati, kupanua ushirikiano wa kikanda kupitia ubia mbalimbali, kuimarisha tafiti na mijadala ya kiuongozi pamoja na kuongeza uwezo wa taasisi na kuhakikisha uendelevu wa kifedha.
Amesema mpango huo umeendelea kujengwa katika misingi miwili mikuu ambayo ni uongozi na maendeleo endelevu, huku ukitambua kuwa maendeleo endelevu ndiyo njia muhimu kwa Afrika kufikia mustakabali wenye ustahimilivu, ustawi na usawa.
Aidha, amesemakuwawezesha viongozi wa Afrika kufanikisha maendeleo endelevu kunahitaji mbinu mpya za kuwajengea uwezo zinazokwenda sambamba na mahitaji na matarajio yanayobadilika kila wakati.
Amesema mkakati huo pia umeainishwa kuwa unaendana na dira na agenda mbalimbali ikiwemo Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050, Agenda 2063 ya Umoja wa Afrika pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs).
“Miongoni mwa maeneo yatakayopewa kipaumbele katika utekelezaji wake ni ubunifu, maendeleo ya uongozi, ushirikishwaji wa makundi mbalimbali, uchumi wa kijani na mageuzi ya kiuchumi. Utekelezaji wa mkakati huu utahitaji uwekezaji wa takribani Dola za Marekani Milioni 45,” amesema na kuongeza
“Pamoja na changamoto zinazokabili sekta ya ufadhili wa maendeleo duniani, Taasisi ya Uongozi imejipanga kutumia mbinu bunifu za kuongeza vyanzo vya fedha na kuwakaribisha wadau mbalimbali kushirikiana katika safari ya kuimarisha uongozi kwa maendeleo endelevu Afrika,” amesema

