NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
MWANARIADHA nyota wa Tanzania, Alphonce Simbu pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari wanatarajiwa kushiriki katika mbio za Wakili Marathon 2026 zitakazofanyika Mei 31, 2026 Viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma, zikiwa na lengo la kuhamasisha utoaji wa msaada wa kisheria kwa jamii.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo Ijumaa Mei 15,2026, Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili wa Serikali (PBA) na waandaaji wa mbio hizo, Ado November amesema maandalizi yote yamekamilika na kwamba mashindano hayo yana hadhi ya kimataifa kutokana na kuzingatia vigezo vinavyotakiwa.
Amesema wanatarajia ushiriki mkubwa wa wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini huku akiwahamasisha kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mbio hizo ambazo pia zitakuwa na vipengele mbalimbali vya burudani na kijamii.
“Tumewaandalia wananchi mbio za viwango vya kimataifa na tunatarajia washiriki zaidi ya 5,000. Hii ni fursa muhimu ya kuhamasisha utoaji wa msaada wa kisheria kwa wananchi,” amesema November.
Ameeleza kuwa viingilio vya ushiriki vitakuwa shilingi 40,000 na 150,000 kulingana na kategori za washiriki, huku washindi wakitarajiwa kupata medali pamoja na zawadi mbalimbali.
Mbali na mbio za watu wazima, amesema pia kutakuwa na mbio maalum kwa ajili ya watoto pamoja na matukio mbalimbali ya burudani yatakayowakutanisha wasanii na viongozi tofauti wa kitaifa.
Ado amesisitiza kuwa kupitia mbio hizo watasaidia jamii kwa kutoa huduma za msaada wa kisheria bure, akibainisha kuwa hadi sasa zaidi ya Watanzania milioni nne katika mikoa nane tayari wamefikiwa na huduma hiyo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Rais wa Chama cha Riadha nchini (RT) na mwanariadha nguli wa Tanzania, Kanali Mstaafu Juma Ikangaa amesema Wakili Marathon 2026 pia itakuwa jukwaa muhimu la kuibua vipaji vipya vya riadha vitakavyoweza kuibua wanariadha wengine watakaoiwakilisha Tanzania katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.
Aidha Ikangaa ameipongeza PBA kwa kukidhi vigezo vyote vya kuandaa mbio hizo za kimataifa huku akisisitiza kuwa RT itaendekea kushirikiana na waandaaji wa mbio hizo ili kuhakikisha wanariadha chikupikizi wanaibuliwa.



