*Yaimarisha kilomita 564 za mpaka na Kenya,
*Yatenga Sh.Bil 1/- mwaka 2026/27 kuharakisha uimarishaji mipaka
*Yatumia teknolojia za satelaiti, GIS na GNSS kuongeza usahihi wa vipimo.
NA MUNIR SHEMWETA
UNAPOSIMAMA katika eneo la Tarakea wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro na kutazama safu za alama za mpaka zikielekea mbali hadi upeo wa macho, unaweza kuona zaidi ya vigingi vya saruji vilivyopandwa ardhini.
Unaona mstari unaobeba historia ya taifa. Unaona alama zinazobainisha mamlaka ya Tanzania, uhuru wake, usalama wake na mustakabali wake.
Katika kipindi hiki ambapo dunia inakabiliwa na changamoto mbalimbali za kiusalama, ongezeko la biashara za kuvuka mipaka, uhamaji wa watu na ushindani wa kiuchumi kati ya mataifa, usimamizi wa mipaka umeendelea kuwa moja ya masuala muhimu katika ujenzi wa dola imara.
Ndiyo maana Tanzania imeendelea kuwekeza katika uimarishaji mipaka yake ya kimataifa kupitia mpango mkubwa unaolenga kuhakikisha mipaka yote ya nchi inalindwa, inatambulika na inasimamiwa kwa mujibu wa sheria na makubaliano ya kimataifa.
Hatua hiyo pia ni sehemu ya utekelezaji Programu ya Umoja wa Afrika ya Uimarishaji Mipaka (African Union Border Programme – AUBP), ambayo inalenga kuhakikisha mipaka yote ya nchi za Afrika imeimarishwa ifikapo mwaka 2027.Tanzania ni moja ya nchi zenye eneo kubwa katika Afrika Mashariki na Kusini, ikiwa imepakana na mataifa 10 ambayo ni Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zambia, Malawi, Msumbiji, Comoro na Shelisheli.
Mipaka hiyo inajumuisha sehemu za nchi kavu, mito, maziwa na bahari.
Kutokana na ukubwa wake, usimamizi wa mipaka hiyo unahitaji uwekezaji mkubwa wa rasilimali, utaalamu na teknolojia ili kuhakikisha kila sehemu inatambulika kwa usahihi.
Kwa miaka mingi, baadhi ya alama za mipaka ziliharibiwa kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo shughuli za kibinadamu, mabadiliko ya mazingira na kukaa kwa muda mrefu bila ukarabati.Hali hiyo ilihitaji hatua za makusudi za serikali kurejesha na kuimarisha alama hizo ili kuondoa sintofahamu zinazoweza kujitokeza katika maeneo ya mipakani.
Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Leonard Akwilapo, katika mwaka wa fedha 2026/27, serikali imeendelea kuongeza kasi ya utekelezaji mradi huo ambapo jumla ya Sh. bilioni moja zimetengwa kwa ajili ya uimarishaji mipaka ili kuhakikisha Tanzania inafikia malengo ya Umoja wa Afrika (AU) kwa wakati.
Anasema kuwa hadi Mei 15, 2026, serikali ilikuwa imeimarisha kilomita 564 za mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Kenya.
“Mafanikio haya yanawakilisha asilimia 75 ya kilomita 758 za mpaka mzima wa nchi kavu kati ya Tanzania na Kenya,” Dk. Akwilapo anasema.
Kwa mujibu wa waziri huyo, kazi hiyo ilijumuisha uwekaji alama mpya za mpaka, ukarabati wa alama zilizoharibika, upimaji wa kisasa wa maeneo ya mipakani pamoja na uandaaji nyaraka na ramani za mipaka.Anasema sehemu iliyokamilishwa hivi karibuni ni eneo la kilomita 106 kutoka Tarakea wilayani Rombo hadi Hifadhi ya Taifa Mkomazi wilayani Mwanga.
“Katika mwaka wa fedha 2026/27, wizara imepanga kuendelea kuimarisha kilomita 140 za mpaka wa Tanzania na Kenya, kilomita 70 za mpaka wa Tanzania na Burundi pamoja na kupima na kuimarisha kilomita 100 za mipaka ya kimataifa katika maeneo ya maji,” Dk. Akwilapo anasema.
Hatua hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Tanzania inalinda mipaka yake kwa viwango vya kimataifa huku ikiimarisha uhusiano mzuri na nchi jirani.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Umoja wa Afrika ya Uimarishaji Mipaka (African Union Border Programme), mpaka wa Tanzania na Kenya ni miongoni mwa maeneo yanayoonesha mafanikio makubwa katika utekelezaji mpango wa uimarishaji mipaka barani Afrika.Hivyo, mpaka wa Tanzania na Kenya umetajwa kuwa moja ya mifano bora ya utekelezaji Programu ya Umoja wa Afrika ya Uimarishaji Mipaka.
Kutokana na mafanikio yaliyopatikana, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ilifanya ziara maalum katika eneo la Holili wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro kujionea maendeleo ya mradi huo.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Timotheo Mzava, alisema kazi iliyofanywa na Wizara ya Ardhi ni kubwa na ya mfano kutokana na ukubwa wa eneo husika pamoja na changamoto za kijiografia zilizokuwapo.
“Kipekee kwenye mpaka huu, ukisimama hapa unaona mpaka kule juu alama zimewekwa. Hii ni kazi kubwa sana. Tunawapongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kazi kubwa waliyoifanya,” Mzava anasema.
Kamati hiyo pia ilisisitiza umuhimu wa serikali kuendelea kutenga fedha za kutosha ili kukamilisha sehemu zilizobaki na kuhakikisha mpaka wote unaimarishwa kwa wakati.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Joseph Ikorongo anasema mafanikio ya Tanzania katika uimarishaji mipaka hayajatokana na juhudi za ndani pekee, bali pia ushirikiano mkubwa kati ya Tanzania na nchi jirani.
“Katika mpaka wa Tanzania na Uganda, nchi hizo mbili zinaendelea na majadiliano ya kuendelea na utekelezaji shughuli za uimarishaji mpaka. Majadiliano haya yamefanywa vikao vya Kamati ya Pamoja ya Wataalamu (JTC) kikiwamo kilichofanyika Bukoba mkoani Kagera hivi karibuni,” Ikorongo anasema.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo Msaidizi Idara ya Upimaji na Ramani, mpaka huo una urefu wa kilomita 397.8 ambapo kilomita 109 ni nchi kavu, kilomita 42.8 ni sehemu ya Mto Kagera na kilomita 246 ni sehemu ya Ziwa Victoria.Kadhalika, Tanzania na Rwanda zimefanya majadiliano ya kufikia makubaliano ya pamoja ya kuimarisha mpaka wenye urefu wa takribani kilomita 230.
Makubaliano hayo yanaweka msingi wa utekelezaji shughuli za pamoja za upimaji, uwekaji alama na usimamizi wa mpaka huo.
Kwa upande wa Burundi, Ikorongo anasema jumla ya kilomita 135 zimekwishaimarishwa na serikali mbili zimefanya mafunzo na ukaguzi wa maeneo ya mpaka ili kuweka msingi wa utekelezaji kazi za uimarishaji mpaka huo.
Tanzania na Msumbiji pia zimekamilisha Km 51 za nchi kavu na zimekamilisha kuandaa mpangokazi kuhusu uhakiki na uimarishaji mpaka wa Mto Ruvuma pamoja na kuendelea kuongeza alama katika sehemu za nchi kavu zinazounganisha mataifa hayo mawili.
Uimarishaji mipaka ya kisasa unahitaji matumizi ya teknolojia za hali ya juu ili kupata matokeo sahihi na yanayokubalika kimataifa.
Kwa kutambua hilo, serikali imeendelea kuwajengea uwezo wataalamu wake kupitia mafunzo balimbali yanayohusisha matumizi ya vifaa vya kisasa vya upimaji (GNSS receivers), teknolojia za satelaiti, mifumo ya taarifa za kijiografia (GIS), picha za anga pamoja na mbinu za kisasa za utunzaji ramani za mipaka.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anthony Sanga, anasema mafunzo hayo yana lengo la kujenga uelewa wa pamoja kati ya wataalamu wa nchi zinazopakana na kuongeza kasi ya utekelezaji miradi ya uimarishaji mipaka.
Kwa mujibu wa wataalamu wa wizara, matumizi ya teknolojia hizo yanasaidia kuongeza usahihi wa vipimo, kupunguza gharama za utekelezaji na kurahisisha uhifadhi wa taarifa muhimu za mipaka.
“Mipaka iliyo wazi na kutambulika vizuri huongeza usalama wa taifa kwa kudhibiti uhalifu wa kuvuka mipaka, biashara haramu, magendo, ujangili na vitendo vingine vinavyoweza kuhatarisha usalama wa nchi,” anasema mkazi wa Tarakea mkoani Kilimanjaro, Mussa Hamis.
Vilevile, uimarishaji mipaka ya kimataifa hupunguza migogoro ya mipaka kati ya nchi jirani au wananchi wanaoishi maeneo ya mpakani kwa kuweka wazi mahali mpaka ulipo.
Kwa upande wa uchumi, Ikorongo anasema mipaka iliyoimarishwa hurahisisha biashara za kuvuka mipaka, usafirishaji wa bidhaa na huduma, uwekezaji na utalii.
Anasema wananchi wanaoishi maeneo ya mipakani pia hunufaika kupitia ajira za muda zinazotokana na utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na elimu ya uzalendo na ushiriki wao katika kulinda mipaka ya kimataifa.
Zaidi ya kuweka alama za mipaka, mradi huu unaimarisha mamlaka ya nchi, unalinda amani na usalama, unaimarisha ujirani mwema, unafungua fursa za kiuchumi na unajenga msingi wa maendeleo endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
*Mwandishi wa Makala haya ni Ofisa Habari Mkuu kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Simu: 0786249844

