NA MWANDISHI WETU
WATENDAJI wa Uchaguzi katika Mikoa ya Mara, Simiyu na Manyara wametakiwa kutoa ushirikiano kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na wadau wa uchaguzi wakati wa kutekeleza majukumu yao ili kufanikisha zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mikoa yao.
Wito huo umetolewa leo Agosti 26, 2024 na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacobs Mwambegele wakati akifungua mafunzo ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa watendaji wa uboreshaji ngazi ya mkoa na halmashauri yaliyofanyika katika mji wa Musoma mkoani Mara.
Jaji Mwambegele amesisitiza kuwa ni muhimu kwa watendaji hao kuhakikisha kuwa wanafuata maelekezo ya Tume na kushirikiana kikamilifu ili kuhakikisha zoezi la uboreshaji linaenda vizuri na kwa ufanisi.
“Ninawasihi muwe na ushirikiano mzuri na wa karibu na Tume wakati wote mtakapokuwa mnatekeleza majukumu yenu na ikiwa mnahitaji ufafanuzi au maelekezo yoyote, msisite kuwasiliana na Tume,” amesema Jaji Mwambegele.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Mbarouk Salim Mbarouk ambaye alifungua mafunzo kama hayo mkoani Simiyu amewataka watendaji hao kutoa ushirikiano kwa mawakala wa vyama vya siasa, asasi za kutoa elimu ya mpiga kura na waangalizi wa zoezi hilo.
Mkoani Manyara, mafunzo kwa watendaji wa uchaguzi ngazi ya mkoa yalifunguliwa na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Asina Omari ambaye amewataka watendaji hao kuzingatia mafunzo hayo ili waweze kuwafundisha Maafisa waandikishaji wasaidizi ngazi ya kata.
“Mafunzo haya yanawajengea umahiri wa kuwafundisha Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Kata ili nao wakatoe mafunzo hayo kwa waendeshaji wa vifaa vya Bayometriki na Waandishi wasaidizi ambao ndiyo watakaohusika na uandikishaji wa wapiga kura vituoni,” amesisitiza Jaji Asina.
Kufanyika kwa mafunzo hayo, ni maandalizi ya kuanza kwa mzunguko wa nne wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambao unajumuisha mkoa wa Mara, Simiyu na baadhi ya halmashauri za Mkoa wa Manyara ambazo ni Halmashauri ya Mji wa Babati na Halmashauri za Wilaya za Babati, Hanang na Mbulu ambapo uboreshaji utaanza tarehe 04 Septemba, 2024 hadi 10 Septemba, 2024 na vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.