NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
MNADHIMU Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Salum Haji Othman amesema mazingira ya sasa ya operesheni za kulinda amani duniani yamekuwa magumu na yenye changamoto nyingi zinazohitaji wataalamu wenye uwezo wa kushughulikia si masuala ya kiusalama pekee, bali pia changamoto za kijamii, kiuchumi na kisiasa zinazochochea migogoro katika mataifa mbalimbali.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Juni 19,2026 wakati wa kufunga mafunzo ya wiki mbili ya walinda amani wa kiraia wanaoshiriki katika operesheni za Umoja wa Mataifa, Luteni Jenerali Othman alisema Tanzania inaendelea kuimarisha uwezo wa rasilimali watu kwa kuandaa wataalamu watakaoweza kufanya kazi kwa ufanisi katika mazingira ya kisasa ya ulinzi wa amani.
Alisema mafunzo hayo yamewajengea washiriki uelewa mpana kuhusu operesheni za kulinda amani, sheria za kimataifa zinazoongoza operesheni hizo, usimamizi wa migogoro, masuala ya jinsia, ushirikiano kati ya raia, jeshi na polisi pamoja na huduma za afya ya akili na msaada wa kisaikolojia.
“Washiriki sasa wamepata maarifa muhimu kuhusu mchango wa watumishi wa kiraia katika operesheni za Umoja wa Mataifa na namna wanavyoweza kushiriki katika uratibu wa shughuli za amani, usuluhishi wa kisiasa, misaada ya kibinadamu na maendeleo katika maeneo yenye migogoro,” alisema.
Mafunzo hayo ya wiki mbili yaliyofanyika kwa udhamini wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) na Serikali ya Japan, yalihusisha washiriki 22 kutoka taasisi mbalimbali za Tanzania na nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Washiriki hao walitoka Jeshi la Polisi Tanzania, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Magereza, taasisi mbalimbali za serikali pamoja na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), huku washiriki wengine wakitoka Malawi, Namibia na Zimbabwe.
Luteni Jenerali Othman alisema mafanikio ya mafunzo hayo yanaonesha dhamira ya Tanzania ya kuendelea kuwa miongoni mwa nchi zinazochangia kikamilifu operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa duniani.
Alisema matokeo ya mafunzo hayo yataongeza idadi ya wataalamu wa kiraia wenye sifa za kushiriki katika misheni za Umoja wa Mataifa na kuimarisha uwezo wa taifa wa kuandaa na kupeleka watumishi waliobobea katika maeneo yenye migogoro.
Aidha, aliishukuru Serikali ya Japan, Umoja wa Mataifa pamoja na wadau wengine wa maendeleo kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kujenga uwezo wa Kituo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania na kuandaa wataalamu wanaokidhi viwango vya kimataifa.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania (TPTC), Brigedia Jenerali George Itang’are alieleza kuwa mafunzo hayo yamewaandaa wahitimu kukabiliana sio tu na changamoto za kiusalama, bali pia masuala ya kijamii, kiuchumi na kisiasa yanayojitokeza katika kipindi cha migogoro na baada ya migogoro kumalizika.
Kwa mujibu wake, mafunzo hayo yamefanikisha malengo yaliyokusudiwa na yanatarajiwa kuongeza idadi ya wataalamu wa kiraia wenye sifa za kushiriki katika operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa, sambamba na kuimarisha uwezo wa Tanzania kuandaa na kupeleka wataalamu waliobobea katika misheni za kimataifa.
Alisema mafanikio ya kozi hiyo yanaonesha ushirikiano imara kati ya Serikali ya Tanzania, Serikali ya Japan na Umoja wa Mataifa katika kujenga uwezo wa Kituo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania na kuandaa wataalamu wa kiraia, polisi na wanajeshi kwa viwango vinavyotakiwa na Umoja wa Mataifa.
“Katika mazingira ya sasa, operesheni za kulinda amani zimekuwa ngumu zaidi kutokana na changamoto mpya za kiusalama na kisiasa. Hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na wataalamu wenye uwezo wa kufanya kazi kwa ushirikiano na ufanisi katika mazingira hayo,” alisema.
Naye mwakilishi wa Serikali ya Japan aliwapongeza washiriki wote kwa kuhitimu mafunzo hayo na kueleza kuwa maarifa na uzoefu walioupata utakuwa nyenzo muhimu katika kuendeleza amani, usalama wa binadamu na maendeleo duniani.
Alisema Japan itaendelea kuunga mkono juhudi za kujenga uwezo wa wataalamu wa kulinda amani kupitia ushirikiano wake na Tanzania pamoja na Umoja wa Mataifa.
Naye mmoja wa wanufaika na mafunzo hayo, ambaye ni Ofisa Kazi Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Vaileth Ndenza alisema kupitia mafunzo hayo wamejifunza kuwa wao kama raia wanaowajibu wa kushiriki kikamilifu katika masuala ya ulinzi wa amani.
Kwa upande wake Mrakibu wa Jeshi la Polisi Tanzania (SP), Adolph Pallangyo alisema na yeye ni miongoni wa wanufaika wa mafunzo hayo ambayo yamewajenga na kuwafundisha kwa kina ni kwa namna gani rai awa kawaida anaweza kushiriki kikamilifu katika jukumu la kulinda amani.

