NA MUNIR SHEMWETA, MLELE
MBUNGE wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amemuomba Mkuu wa wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi Alhaji Majid Mwanga kuunda Tume ya Kupitia Mapato na Matumizi ya fedha za Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) katika Halmashauri ya Mpimbwe ili kubaini kama kuna ubadhilifu basi wahusika wachukuliwe hatua kali.
Aidha, amemuomba Mkuu huyo wa wilaya ya Mlele kuchunguza kiasi cha fedha Milioni 44 /-kilichotolewa na Mkandarasi anayejenga barabara ya Kibaoni hadi Sitalike zinazodaiwa kulipwa kwa kijiji bila kufuata utaratibu.
Pinda ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti Aprili 12, 2024 wakati wa mikutano yake ya hadhara na wananchi wa vijiji vya Mirumba, Ilalangulu na Kibaoni katika Halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi.
Kauli ya Pinda inakuja mara baada ya kubadilishwa uongozi wa Kamati ya Kusimamia WMA ndani ya mwezi mmoja tu kamati ilifanikiwa kukusanya Sh. Milioni 200 tofauti na kamati iliyokaa kwa zaidi ya miaka kumi na kudaiwa kutosaidia maendeleo yoyote ya vijiji husika.
“Iundwe tume ya kupita kitabu kwa kitabu tujue miaka 20 fedha zetu zilienda wapi za wananchi hao, wiki mbili milioni 200 hebu tuwaulize miaka 20 wameleta nini?” alihoji Pinda.
“Pia kuna ubadhilifu wa Milioni 44 zilizotolewa na mkandarasi anayejenga barabara ya kiabaoni- Sitalike ambaye amelipa fedha kwa kijiji bila utaratibu. Uchunguzi nani amechukua fedha taslimu ambazo hazijulikani zilipokwenda wapi ufanyike”. amesema Pinda.
Aidha, ameuelezea mpango wa WMA kama wenye faida kubwa kwa vijjji vinavozunguka hifadhi na kutolea mfano wa wilaya ya Tanganyika kama wilaya inayonufaika na mpango huo ambapo kwa mujibu wa Mhe. Pinda mwaka huu wa 2024 vijiji vinavyozunguka hifadhi vinaenda kupokea Sh.Bilioni 16 /-.
Amesema kuwa, kiasi chochote cha fedha kitakachopatikana kupitia mpango wa WMA lazima wananchi wahusishwe matumizi yake ili fedha zinazokusanywa ziende kutumika kwenye shughuli za maendeleo ya vijiji husika.
Mkuu wa wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi Alhaji Majid Mwanga ameahidi kuunda haraka Tume itakayohusisha vyombo vya ulinzi na usalama kama vile TAKUKURU, Jeshi la Polisi na Magereza ili kubaini kama upo ubadhilifu wowote wa fedha za umma basi wahusika waweze kuchukuliwa hatua stahiki.
“Hakuna atakayepona katika suala hilo na lazima tutawashughulikia wahusika wote waliowaibia wananchi. Kazi hii tunaiweza na hatutacheka na mtu hata mmoja”. amesema Alhaji Mwanga.
Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Jamii (WMA) katika Halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele inahusisha vijiji vya Kibaoni, Mirumba, IIalangula pamoja na kijiji kimoja kutoka wilaya ya Nkasi.