NA MWANDISHI WETU,PERTH,AUSTRALIA
TANZANIA imeendelea na mkakati wa kuwaalika wawekezaji wa kimataifa kutumia fursa zilizopo katika Sekta ya Madini nchini, kwa kuwa Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji, kuongeza taarifa za kijiolojia na kuendeleza miradi mikubwa ya madini yenye uwezo wa kuongeza thamani ya uchumi wa taifa.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa, leo Alhamisi Septemba 03, 2026, mjini Perth, Australia wakati akizungumza katika Mkutano wa 24 wa Africa Down Under 2026 ambapo amesema Tanzania imefika kwenye jukwaa hilo ikiwa na ujumbe ulio wazi. “Tuna madini. Tunawekeza katika maarifa na uendelezaji wa ujuzi; tunaboresha mazingira ya uwekezaji; na tuko tayari kushirikiana na wawekezaji.” amesema Kiruswa.
Amesema Sekta ya Madini imeendelea kuwa injini muhimu ya uchumi wa Tanzania, ambapo mchango wake katika Pato la Taifa umefikia asilimia 10.3 mwaka 2025, huku ikichangia takribani asilimia 53 ya thamani ya mauzo yote ya nje ya nchi. Aidha, uzalishaji wa dhahabu uliongezeka hadi takribani tani 68 mwaka 2025 kutoka tani 61.7 mwaka 2024. Dkt. Kiruswa amesema mafanikio hayo yanaakisi mageuzi ya kisera, uwekezaji katika miundombinu na kuongezeka kwa imani ya wawekezaji nchini.
Akizungumzia madini muhimu na ya kimkakati, Dk. Kiruswa amesema Tanzania imekamilisha Mkakati wa Madini Muhimu na ya Kimkakati unaojumuisha kinywe, nikeli, lithiamu, heliamu, kobalti, titanium, shaba, aluminium, niobium na madini adimu ya ardhini (REE’s).
Amesema dhamira ya Serikali sio kuuza madini ghafi, bali kujenga minyororo ya thamani kupitia uchakataji na uongezaji thamani wa madini nchini, sambamba na kuchangia mahitaji ya soko la dunia katika ugavi wa nishati safi.
Dk. Kiruswa pia ameeleza hatua zinazochukuliwa na Serikali kupunguza hatari za uwekezaji katika utafiti wa madini kupitia Mfuko wa Utafiti wa Madini, ambapo asilimia 10 ya mapato yatokanayo ya madini yataelekezwa kwenye tafiti za kijiolojia na kubainisha kuwa GST imefikia asilimia 98 ya uchoraji wa ramani za kijiolojia nchini, na kwamba Serikali inalenga kuongeza utafiti wa kina kutoka takribani asilimia 16 zilizopo hadi kufikia asilimia 50 ya nchi kabla ya mwaka 2030.
Akitoa ushahidi wa fursa zilizopo, Dkt. Kiruswa amesema Mradi wa Dhahabu wa Nyanzaga umefikia takribani asilimia 65 ya utekelezaji na unatarajiwa kuanza uzalishaji katika robo ya kwanza ya mwaka 2027.
Pia ametaja Kabanga Nickel, ambako mazungumzo ya uwekezaji unaozidi Dola milioni 500 yanaendelea; Mahenge Graphite, inayotarajiwa kuanza uzalishaji wa kibiashara mwaka 2028; na Panda Hill Niobium, pamoja na shughuli zinazoendelea katika migodi ya Geita, North Mara na Bulyanhulu.
Kwa upande wa mazingira ya uwekezaji, amesema Serikali imeendelea kufanya mageuzi yanayolenga kuongeza uhakika, utabirika, ufanisi na uwazi, yakiwemo maboresho ya Framework Agreements, mfumo wa kidijitali wa utoaji wa leseni za madini, kuimarisha local content na kuongeza masoko pamoja na vituo vya ununuzi wa madini.
Aidha, Tanzania inatoa vivutio mbalimbali kwa wawekezaji, ikiwemo asilimia 100 ya ukataji wa matumizi yanayokidhi vigezo ya mtaji na utafiti, asilimia 16 ya hisa za Serikali katika miradi inayokidhi vigezo na mifumo ya dhamana za mikopo kwa wachimbaji wanaostahili.
Pia, Dk. Kiruswa amewataka wawekezaji kuja Tanzania na kujionea fursa zilizopo, akisisitiza kuwa Serikali iko tayari kusikiliza mahitaji yao na kushirikiana nao katika kuondoa vikwazo vya uwekezaji.
Amesema Tanzania ina rasilimali, inawekeza katika maarifa, inaboresha mazingira ya uwekezaji na iko tayari kujenga ubia wa kibiashara huku akiwaalika wawekezaji kushiriki Mkutano wa Kimataifa wa Uwezekaji katika Sekta ya Madini Tanzania (Tanzania Mining and Investment Conference – TMIC) 2026, utakaofanyika Novemba 19–21, 2026 jijini, Dar es Salaam.





