NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
TANZANIA inapoelekea uchumi wa kidijitali, matumizi ya fedha tasilimu yanaanza kupata ushindani mkubwa kutoka kwa mifumo ya malipo ya kielektroniki nchini.
Serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo wameendelea kusisitiza matumizi ya teknolojia katika biashara na huduma za kifedha.
Hata hivyo, wakati mijini huduma za malipo kwa njia ya simu, benki na mifumo mingine ya kidijitali zinazidi kuzoeleka, bado kuna swali muhimu linalohitaji majibu: Je, Tanzania inaweza kufikia uchumi usiotegemea fedha tasilimu bila kuhakikisha wananchi wa vijijini wanawezeshwa kushiriki kikamilifu katika mfumo huo?
Swali hilo linapata uzito kutokana na ukweli kwamba sehemu kubwa ya shughuli za kiuchumi vijijini bado hutegemea fedha taslimu. Mkulima anapouza mazao, mfanyabiashara anapouza bidhaa dukani au mwananchi anapofanya manunuzi sokoni, fedha taslimu bado ni njia inayotumika kwa kiwango kikubwa.
Kwa hiyo,azma ya kupunguza matumizi ya fedha taslimu (cash) haiwezi kutegemea mabadiliko ya tabia za wananchi pekee. Inahitaji pia kubadilisha mazingira yanayowafanya wananchi waendelee kuitegemea.
Mjadala wa biashara ya kidijitali
Mnamo Julai 30 na 31, 2026, zaidi ya wadau 80 kutoka sekta ya umma, sekta binafsi na washirika wa maendeleo walikutana jijini Dar es Salaam katika Mjadala wa Wadau wa Biashara Mtandao (E-Commerce) wenye kaulimbiu “Kuimarisha Biashara ya Kidijitali Tanzania.”
Mjadala huo uliandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) ulidumu kwa siku mbili na katika kipindi chote hicho washiriki walijadili kwa kina masuala ya sera, kanuni, miundombinu ya kidijitali, biashara ya mipakani, ubunifu, upatikanaji wa masoko na mifumo ya malipo ya kielektroniki.
Wadau walibainisha kuwa biashara ya mtandao ina nafasi kubwa katika kukuza uchumi wa kidijitali, kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani, kikanda na kimataifa, pamoja na kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati.
Lakini pia walitaja changamoto ambazo bado zinahitaji kushughulikiwa, ikiwemo miundombinu hafifu ya kidijitali, ukosefu wa uratibu wa kutosha kati ya wadau, mifumo isiyoratibiwa ya malipo ya biashara mipakani na kutokuwepo kwa uhakika wa baadhi ya kanuni zinazosimamia biashara za kidijitali.
Changamoto hizo zinaibua hoja nyingine muhimu: ikiwa bado kuna maeneo yenye changamoto za miundombinu ya kidijitali, Tanzania itafikaje kwenye uchumi usiotegemea fedha taslimu?
Vijijini ndipo mtihani ulipo
Uhalisia wa vijijini unaonyesha kuwa safari ya kutoka katika mfumo wa kutoa fedha taslimu kwenda kidijitali si rahisi kama kuhamasisha wananchi kutumia simu kufanya malipo.
Mwananchi anaweza kuwa na simu, lakini je, ana mtandao wa uhakika? Anaweza kuwa na huduma ya fedha kwa njia ya simu, lakini je, anapata wakala kwa urahisi? Au Anaweza kuwa tayari kutumia malipo ya kidijitali, lakini je, mfanyabiashara anayemnunulia bidhaa anakubali malipo hayo?
Maswali hayo yanaonyesha kwamba cashless economy ni mfumo mzima, unaohitaji miundombinu, elimu, uaminifu, gharama nafuu na upatikanaji wa huduma.
Kwa mfano, mkulima anaweza kuuza mazao yake na kuamua kulipwa kwa njia ya simu. Lakini ikiwa baada ya kupata fedha hizo anahitaji kwenda kwa wakala ili kuzitoa kwa ajili ya matumizi ambayo hayawezi kulipwa kidijitali, bado mfumo huo utamrudisha kwenye cash.
Hivyo, tatizo si tu kumshawishi mwananchi kupokea fedha kidijitali, bali kuhakikisha kwamba anaweza kutumia fedha hizo kidijitali katika maisha yake ya kila siku.
Mtandao na umeme ni msingi
Moja ya changamoto kubwa katika safari hii ni upatikanaji wa miundombinu ya mawasiliano. Malipo ya kidijitali yanahitaji mtandao unaopatikana kwa wakati unaohitajika. Mtandao unapokuwa dhaifu au kukatika, muamala unaweza kushindikana na kumfanya mwananchi kurejea kwenye fedha taslimu.
Hali hiyo inaweza kuwa changamoto zaidi kwa wafanyabiashara wadogo ambao biashara zao zinategemea miamala ya kila siku.
Umeme nao ni sehemu ya mjadala. Simu zinahitaji kuchajiwa na mifumo ya kidijitali inahitaji miundombinu inayofanya kazi muda wote. Kwa hiyo, Tanzania inapozungumzia uchumi wa kidijitali, suala la nishati na mawasiliano haliwezi kutenganishwa na suala la malipo ya kidijitali.
Uaminifu ni msingi wa cashless economy
Mbali na miundombinu na kuna suala la uaminifu. Baadhi ya wananchi wanaweza kuendelea kuamini zaidi fedha iliyo mkononi kuliko salio lililo kwenye simu. Hofu ya kutuma fedha kwa namba isiyo sahihi, kutapeliwa, kupoteza simu, kusahau namba ya siri au muamala kukwama inaweza kuwafanya wananchi kusita kutumia huduma za kidijitali.
Ndiyo maana hatua za kuongeza matumizi ya malipo ya kielektroniki zinapaswa kwenda sambamba na mifumo madhubuti ya ulinzi wa mtumiaji, elimu ya fedha na huduma rahisi za kushughulikia malalamiko.
Kwa upande mwingine, wanahitaji pia kuelimishwa namna ya kuthibitisha malipo ili wasitegemee ujumbe wa simu pekee au kuingia kwenye hatari ya utapeli.
Aidha Tanzania inapojenga uchumi wa kidijitali, mafanikio yake hayatakiwi kupimwa kwa kuangalia matumizi ya huduma hizo Dar es Salaam, Arusha, Mwanza au miji mingine pekee.
Mafanikio ya kweli yataonekana pale ambapo mkulima kijijini anaweza kuuza mazao yake na kulipwa kidijitali, mama lishe anaweza kupokea malipo kwa simu, duka la kijijini linaweza kufanya miamala bila kutegemea cash pekee, na mwananchi anaweza kutumia fedha zake za kidijitali kulipia huduma mbalimbali bila kulazimika kuzitoa kuwa fedha taslimu.
Kwa maana hiyo, cashless Tanzania inahitaji zaidi ya teknolojia; inahitaji mazingira yanayomfanya mwananchi achague digital kwa sababu ni rahisi, salama, nafuu na inapatikana.
Serikali na sekta binafsi wana jukumu gani?
Ili kufikia azma hiyo, Serikali na sekta binafsi wanahitaji kuendelea kufanya kazi kwa pamoja, kama ilivyosisitizwa katika mjadala wa wadau wa biashara mtandao.
Kipaumbele kinapaswa kuwa kuboresha miundombinu ya mawasiliano na nishati, kupunguza vikwazo vya matumizi ya huduma za kidijitali, kuongeza elimu ya fedha na teknolojia, kuimarisha ulinzi wa watumiaji na kuweka mazingira yatakayowafanya wafanyabiashara wadogo kukubali malipo ya kielektroniki.
Aidha, mifumo ya malipo inapaswa kuwa rahisi na yenye kuaminika, huku taasisi zinazohusika zikihakikisha kwamba wananchi wanapata msaada wa haraka pale wanapokutana na changamoto.
Hitimisho
Azma ya kupunguza matumizi ya fedha taslimu ni sehemu ya mabadiliko makubwa kuelekea uchumi wa kidijitali. Hata hivyo, safari hiyo haitafanikiwa kwa kuwaambia wananchi waache cash bila kuwaandalia mazingira mbadala yanayofanya kazi.
Kwa wananchi wa mijini, malipo ya kidijitali yanaweza kuonekana kuwa jambo la kawaida. Lakini kwa mwananchi wa kijijini, bado kuna maswali kuhusu mtandao, umeme, mawakala, gharama, elimu na uaminifu.
Kwa hiyo, changamoto kubwa si kumshawishi mwananchi kuacha cash; changamoto ni kujenga mfumo ambao utamfanya asihitaji cash kwa kila hatua ya maisha yake ya kiuchumi.
Hapo ndipo mjadala wa biashara mtandao, malipo ya kielektroniki na uchumi wa kidijitali unapaswa kuanzia—si kwenye teknolojia pekee, bali kwenye maisha halisi ya mwananchi anayetarajiwa kuitumia.
Tanzania ya cashless itafanikiwa pale ambapo teknolojia itamfikia mwananchi wa mwisho, si mwananchi wa mjini pekee.

