NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
RAIS Samia Suluhu Hassan amezindua Tume ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai itakayochunguza kwa kina matukio ya uvunjifu wa amani na ghasia zilizotokea wakati na baada ya uchaguzi wa Oktoba 2025
Tume hiyo inakuja kutokana na mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Rais iliyoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman ambayo pamoja na masuala mengine ilipendekeza kufanyika kwa uchunguzi wa kina ili kubaini wahusika wa matukio hayo na hatua stahiki za uwajibikaji zichukuliwe.
Akizungumza katika uzinduzi wa tume hiyo Ikulu jijini Dar es Salaam leo, Rais Samia amesema tume hiyo imepewa muda wa miezi mitano kukamilisha majukumu yake na kisha kuwasilisha ripoti rasmi
Amesema anamshukuru Mwenyekiti na makamishna wa tume hiyo kwa kukubali kuifanya kazi hiyo kwa maslahi mapana ya Taifa na wananchi kwa ujumla.
“Niwaombe watanzania kutoa ushirikiano unaohitajika, tuisaidie tume hii iweze kufanya kazi yake, niwashukuru makamishna na mwenyekiti wa tume hii kwa kukubali jukumu hili zito,” amesema Rais Samia
Tume hiyo imeundwa na wajumbe sita ambao wajumbe wanne wanatoka Tanzania, mmoja akitoka nchini Uganda na mmoja akitoka Jmahuri ya Namibia.






