NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
WACHIMBAJI Wadogo wa madini nchini wanatarajiwa kunufaika na fursa mpya za mitaji, vifaa vya kisasa na teknolojia za uchimbaji kufuatia mpango wa kampuni ya Falcone Sovereign Wealth Fund Partnership Inc. kutoka Marekani kuwekeza nchini kupitia ushirikiano wa moja kwa moja na wachimbaji wadogo wa madini.
Hayo yalibainishwa Agosti 4, 2026, wakati viongozi wa Kampuni hiyo walipokutana na Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa, jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujadili namna ya kutekeleza ushirikiano huo.
Akizungumza katika kikao hicho, Dk. Kiruswa aliipongeza Kampuni ya Falcone kwa uamuzi wake wa kuelekeza uwekezaji kwa wachimbaji wadogo wa Kitanzania, akieleza kuwa hatua hiyo ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Alisema uwekezaji unaolenga kuwawezesha wachimbaji wadogo una faida kubwa kwa kuwa mapato yanayotokana na shughuli hizo hubaki ndani ya nchi, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kuimarisha ustawi wa Watanzania.
Aidha, Dkt Kiruswa alisisitiza kuwa Kampuni hiyo inapaswa kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia kikamilifu Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Serikali inayosimamia sekta ya madini nchini.
Alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kupitia sera na sheria rafiki zinazowezesha kampuni za ndani na nje kushirikiana na wachimbaji wadogo kwa manufaa ya pande zote.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Falcone Sovereign Wealth Fund Partnership Inc., Nicholas Dalessandro, alisema Kampuni hiyo itaanza utekelezaji wa mpango wake kwa kushirikiana na wachimbaji wadogo wa eneo la Chunya, kabla ya kupanua wigo wa shughuli zake katika maeneo mengine nchini.
Alibainisha kuwa mbali na kutoa mitaji, vifaa na teknolojia, Kampuni hiyo inalenga kuwawezesha wanawake, vijana na makundi maalumu yanayojishughulisha na shughuli za madini ili kuongeza tija, usalama na mchango wao katika maendeleo ya sekta hiyo.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, pamoja na viongozi wengine wa Wizara na Kampuni hiyo.




