NA MWANDISHI WETU, MBINGA
NAIBU Waziri wa Nishati Judith Kapinga amewasha kwa mara ya kwanza umeme kwenye kijiji cha Litumbandyosi, Kata ya Litumbandyosi kwenye Halmashauri ya wilaya ya Mbinga Oktoba 8, 2023.
Kapinga amesema, umeme ambao umefika kwa mara ya kwanza katika kijiji hicho ni haki ya Wananchi hao kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Dk Samia Suluhu Hassan, ilitenga fedha kwa muda mrefu na kuwataka Wananchi hao kuchangamkia fursa ya kujiunga na huduma hiyo ili kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Ameeleza kuwa kati ya fedha hizo, Wilaya ya Mbinga imepewa shilingi bilioni 28.8 kwa ajili ya Miradi hiyo ambapo kwa Kata ya Litumbandyosi na kijiji cha Litumbandyosi pekee yake Mkandarasi wa Kampuni ya NAMIS Corporate LTD ametumia Sh. Milioni 971 kukamilisha Mradi huo ambao Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga ameuwasha.
“Wananchi wa Litumbandyosi ni haki yenu kupata umeme na Serikali ilishatenga fedha kupitia Mradi wa Kupeleka Umeme Vijijini wa Awamu ya Tatu na Mzunguko wa Pili chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA); fursa hii, ilitengewa fedha, zaidi ya mwaka mmoja ulilopita”. alisema Kapinga.
“Mhe. Rais ametoa fedha mpate umeme, mtapata umeme. Niwahakikishie ndugu zangu wa Kingoli, umeme unakuja, tutamsimamia Mkandarasi kuhakikisha nguzo zinakuja na umeme unawasha, ili na ninyi pia mpate umeme. Hatutawaangusha, tutahakikisha mnapata umeme,” amesema Naibu Waziri, Kapinga.
Ameendelea kusema kuwa,Rais ametoa fedha kwa vijiji vyote vya Tanzania ambavyo bado havijapata umeme, ili vipate umeme ikiwemo vijiji vinne (4) vya Kata ya Litumbandyosi vilivyopo katika wilaya ya Mbinga na kuongeza kuwa jumla ya Sh. Bilioni 2.07 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo.
Kapinga amesema kuwa Serikali, itapeleka umeme katika maeneo yote, yenye shughuli za kijamii na kiuchumi, zikiwemo taasisi kama shule, vituo vya afya, misikiti, na makanisa.
Amesema kuwa kati ya fedha hizo, Wilaya ya Mbinga imepewa shilingi bilioni 28.8 kwa ajili ya Miradi hiyo ambapo kwa Kata ya Litumbandyosi na kijiji cha Litumbandyosi pekee yake Mkandarasi Kampuni ya NAMIS Corporate LTD ametumia shilingi milioni 971 kukamilisha Mradi huo ambao Naibu Waziri ameuwasha.
Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Nishati, Kapinga amewaahidi Wananchi wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma ambao vijiji vyao bado havijafikiwa na huduma ya umeme kwamba watahakikisha vijiji hivyo, vinapata umeme kabla ya mwezi Desemba 30, 2023.
Kutokana na umuhimu wa nishati hiyo ya umeme vijijini ,Meneja huyo aliahidi kwamba ifikapo Desemba 30 mwaka huu jumla ya viijiji 45 vya Mbinga vijijini vitakuwa na umeme wa kawaida.
Hata hivyo Naibu Waziri Kapinga alimtaka. Mhandisi, Shaidu Rutakolezibwa, Meneja Miradi kutoka kampuni ya NAMIS Corporate Ltd (Mkandarasi) anayetekeleza mradi huo wilaya ya Mbinga kuwaeleza Wananchi ni lini atakamilisha kazi ya kufikisha umeme kwa Wananchi hao.
Katika hatua nyingine , Kiasi cha Sh.Bilioni 91.2 zimetengwa na Mkoa wa Ruvuma kwa ajili ya kukamilisha miradi ya nishati ya umeme vijijini katika Mkoa huo.
Hayo yamebainishwa Jumapili Oktoba 8, 2023 na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi, Yusuph Ismail ambaye pia ni Meneja Uthibiti na Ufuatiliaji wa Miradi ya REA.
Naye Mhandisi, Ismail ameongeza kuwa katika fedha hizo Mbinga vijijini imepata Sh. Bilioni 19.8 na Mbinga mjini imepata shilingi bilioni 9.
“Kwa upande wa Mbinga vijijini, Mkandarasi anatarajia kupeleka umeme vijiji 45 vilivyobaki hdi kufikia Desemba 30, 2023” amesema Mhandisi Ismail.







