NA DANSON KAIJAGE,SIMIYU
JUMLA ya Sh.Bilioni 16.2 zimetolewa na Serikali kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi ambao wanapitiwa na barabara nchini.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Simiyu ya ukaguzi wa miradi ya barabara na kuzungumza na wananchi sambamba na wakandarasi.
Bashungwa amesema kuwa Rais, Dk Samia Suluhu Hassan ametoa kibali cha Sh. Bilioni 16.2 kwa ajili ya malipo ya fidia za wananchi wanaopisha ujenzi wa miradi ya barabara kote nchini.
Bashungwa amesema hayo mkoani Simiyu mara baada ya kukagua mtandao wa barabara mkoni humo na kujionea utelelezaji wa ujenzi wa barabara ya mchepuo (Maswa Bypass) yenye urefu wa kilometa 11.3 kwa kiwango cha lami ambao ujenzi umefikia asilimia 99.
“Mheshimiwa Rais ameshatoa zaidi ya Bilioni 16 kwa ajili ya kulipa madeni ya fidia ya kuishia Juni 30, 2023, dhamira ya dhati aliyo nayo ni kuhakikisha mtandao wa barabara nchini unaimarishwa”, amesema Bashungwa.
Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa lengo la Serikali la kuijenga barabara ya mchepuo ya Maswa (Maswa Bypass) ni kupunguza msongamano wa magari yanayopita katikati ya mji wa Maswa.
Amesema Serikali tayari imetenga fedha kwa ajili ya kuanza upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa bararara ya Bariadi-Salama-Mhayo-Magu (km 76), Bariadi-Itilima-Mwandoya-Moroco (km 104), Nyashimo-Ngasamo-Ndutwa (km 48) ili kupata gharama za ujenzi wake kwa kiwango cha lami.
Akitoa taarifa ya mradi, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Simiyu Mhandisi John Mkumbo ameeleza kuwa mkataba wa ujenzi wa barabara hii ulitiwa saini kati ya TANROADS na Mkandarasi kampuni ya CHICO Juni Mosi t, 2021 kwa gharam ya Sh.Bilioni 13.4.
Ameongeza kuwa mkandarasi anaendelea kumalizia kazi ndogo ndogo za kuweka alama za barabarani, kuchora mistari ya usalama barabarani pamoja na kujenga miundombinu saidizi ya barabara.