NA MWANDISHI MAALUMU, DAR ES SALAAM
WAFANYAKAZI wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamefanya utalii wa ndani wa kutembelea msitu wa mazingira asilia Pugu Kazimzumbwi uliopo Kisarawe mkoani Pwani.
Akizungumzia kuhusu utalii huo Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dk. Peter Kisenge alisema wafanyakazi wa Taasisi hiyo siku ya Jumamosi waliamua kuunga mkono jitihada za Rais Dk.Samia Suluhu Hassan za kuhamasisha utalii na kwenda kufanya utalii wa ndani katika msitu huo.
Dk. Kisenge alisema wafanyakazi wa JKCI wanafanya kazi katika mazingira ya huruma ya kuwahudumia wagonjwa wenye matatizo mbalimbali kwa kufanya kwao utalii katika msitu huo kumewafanya wajifunze vitu vingine vipya tofauti na vile wanavyokutana navyo kazini pamoja na kujiburudisha.
“Tumewaleta wafanyakazi wetu kutalii katika msitu huu na kuona mazingira tofauti na yale waliyopo kila siku ya kuwahudumia wagonjwa kwa kufanya hivi kutawapa ari mpya ya kufanya kazi pamoja na kutangaza utalii uliopo kwa wagonjwa tunaowahudumia kwani Taasisi yetu ina wahudumia wagonjwa wengi kutoka nje ya nchi “, alisema Dk Kisenge.
Kwa upande wake muongoza watalii kutoka Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Magdalena Lukumay alisema siku ya Jumamosi waliwapokea watalii wa ndani kutoka JKCI ambao walitembelea msitu huo na kuona vivutio mbalimbali vilivyopo.
Lukumay alisema ni mara chache wanapokea kundi kubwa lenye watalii wengi wa ndani kama ilivyotokea kwa JKCI na kuziomba Taasisi nyingine za Serikali na zisizo za Serikali kuiga mfano huo na kuwapeleka wafanyakazi wao kufanya utalii wa ndani katika msitu huo.
“Katika msitu huu wa mazingira asilia wenyeji waliopo ni kabila la Wazaramo, kuna shughuli mbalimbali zinazofanyika hapa hii ikiwa ni pamoja na ngoma za asili, matambiko yanayofanyika katika mapango ya mzimu wa Mavoga na vyakula vya asili”, alisema .
Nao wafanyakazi wa JKCI ambao walitembelea msitu wa mazingira asilia Pugu Kazimzumbwi walishukuru kwa nafasi waliyoipata na kusema kuwa imewasaidia kujifunza vitu vipya ambavyo hawakuwa wanavifahamu.
Theresia Marombe ambaye ni Ofisa Muuguzi wa JKCI alisema amefurahi kutembelea msitu huo na ni mara yake ya kwanza kufika mahali hapo amefurahi zaidi kuona wafanyakazi wote wamekaa pamoja katika mazingira ya asili na kujifunza mambo mbalimbali.
“Kuna umuhimu wa watanzania kutenga muda wa kutembelea vivutio vya utalii tulivyonavyo na kuona vitu vya asili , kuja hapa ni mara yangu ya kwanza nitawaambia na wenzangu waje hapa kuona miti, popo na ndege wa asili waliopo hapa”, alisema Marombe
“Ninashukuru kupata nafasi ya kutembelea msitu wa mazingira asilia Pugu Kazimzumbwi nimeona vitu ambavyo mjini havipo lakini hapa vipo, ninatoa wito kwa watanzania wenzangu wafanye utalii wa ndani kama huu tulioufanya siku ya leo na kuona vitu vizuri ambavyo Mwenyezi Mungu ametujalia Watanzania kuwa navyo”, alisema Herry Magwaza ambaye ni Mtunza Kumbukumbu wa JKCI.
Wakiwa katika msitu huo wafanyakazi hao walipata nafasi ya kutembelea maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na bwawa la Minaki lenye kina cha mita nane na urefu wa kilomita 1.2, mapango ya popo, pango la mzimu wa Mavoga, kupanda mlima wenye urefu wa kilomita 1.5 kwa kutumia kamba pamoja na kuona miti ya asili , ndege, vipepeo na panzi wenye bendera ya taifa .