NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WAGONJWA 310 kutoka nchi za Somalia, Malawi, Kenya, Rwanda, Visiwa vya Comoro, Ethiopia, Burundi, Armenia, Norway na Uingereza wamepata huduma za kibingwa za matibabu ya moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kamati za utalii tiba zilizopo katika Hospitali za kibingwa hapa nchini Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dk Peter Kisenge alisema wagonjwa hao wamepata matibabu hayo kwa kipindi cha miaka mitatu.
Mkurugenzi huyo Mtendaji ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema JKCI katika kuhamasisha utalii tiba mwaka jana imeshiriki maonyesho ya huduma inazozitoa katika visiwa vya Como, wiki hii wataalamu wa Taasisi hiyo wako nchini Malawi kwa ajili ya kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo na baadaye inatarajia kwenda nchini Burundi na Jamhuri ya watu wa Congo kutoa huduma hizo.
Dk. Kisenge alisema katika Taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu kumekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa wanaotoka nje ya Tanzania, kwa mwaka 2022 waliona wagonjwa zaidi ya 200 na mwaka huu wa 2023 hadi sasa wametoa huduma kwa wagonjwa 110.
“JKCI imetengeneza mpango mkakati ambao unafuata malengo yaliyowekwa na kamati ya kitaifa ya utalii tiba kuhakikisha kwamba kupitia sekta ya afya utalii unaongezeka hapa nchini”,.
“Ninaipongeza kamati ya kitaifa ya utalii tiba kwa kuwa chachu ya kufanikisha malengo ya Rais wa Serikali ya awamu ya sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ninaahidi Taasisi yetu imejipanga kutangaza utalii tiba kwa vitendo”, alisema Dk.Kisenge.
Aidha Dk. Kisenge amesema kuwa JKCI inatarajia kufanya mkutano mkubwa mwaka 2024 utakaoonesha nini kinafanywa na Taasisi hiyo na matarajio yao ni kuhakikisha kuwa zaidi ya nchi 40 zinashiriki katika mkutano huo.
Akizungumza mara baada ya kuzindua kamati za utalii tiba Mratibu wa matibabu nje ya nchi kutoka Wizara ya Afya Dk Asha Mahita alisema hospitali za kibingwa zinatakiwa kujenga uaminifu na ukarimu kwa wagonjwa wanaowahudumia ili kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda nje ya nchi kutibiwa kwani huduma zote za kibingwa sasa hupatikana hapa nchini.
Dk.Mahita alisema dhana ya utalii tiba nchini ilikuwa bado haijaeleweka vizuri hapo awali lakini tangu kuanza kwa kamati maalum ya utalii tiba mabadiliko makubwa yametokea kwani sasa wagonjwa kutoka nchi nyingi za Afrika wanakuja Tanzania kupata huduma za matibabu ya kibingwa yanayotolewa na Hospitali zetu.
Dk.Mahita alisema lengo kubwa la utalii tiba ni pamoja na kuongeza pato la nchi lakini pia mtu mmoja mmoja katika nchi kufaidika kupitia utalii tiba kwani wagonjwa wanaofika watahitaji malazi na huduma nyingine hivyo wote kwa pamoja kukuza uchumi wa nchi na uchumi binafsi.
“Kuzindua kamati za utalii tiba ni tukio kubwa katika sekta ya tiba utalii hapa nchini, nawapongeza kwa niaba ya Wizara kwa kazi kubwa ambayo kamati ya kitaifa ya utalii tiba imefanya tangu walipoteuliwa mwaka 2021 hadi sasa”, alisema Dk. Mahita
Aidha Dk Mahita amezitaka Hospitali zote nchini kujitathmini na kuamua zinataka kufanya nini ili kuendana na malengo ya wizara inapojiandaa kutengeneza muongozo ambao utaleta majukumu ya kada zilizopo katika Hospitali kuwezesha kila mfanyakazi kuchukua nafasi yake na kutekeleza majukumu yake.
Naye Mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya utalii tiba Prof. Mohamed Janabi alisema kupitia kamati ya kitaifa ya utalii tiba wameweza kuujulisha umma nini maana ya utalii tiba hivyo kupunguza idadi ya watu waliokuwa wanakwenda nje ya nchi kwa ajili ya kupata huduma za matibabu.
Prof. Janabi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili alisema kufikia mwaka 2030 Tanzania inatarajia kuwa na watalii milioni tano waonafika hapa nchini kwa mwaka na kupitia watalii hao wapo baadhi ambao watahitaji huduma za matibabu hivyo ni vyema Hospitali zikaendelea kuboresha huduma na kuvitunza vizuri vifaa tiba kwani ni vya gharama.
“Dhumuni letu kubwa kama kamati tunataka tupate angalau asilimia 10 ya wagonjwa wanaokwenda nchi za ulaya kwaajili ya matibabu kutibiwa katika nchi yetu kwasababu sasa vifaa tunavyo na wataalam kwaajili ya kutoa huduma za kibingwa wapo wakutosha”, alisema Prof. Janabi.