NA MWANDISHI WETU, PWANI
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), Bagamoyo mkoani Pwani, kimemtaka Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Halima Okash kusimamia utatuzi wa kero ya uwepo wa tembo katika kata ya Kiwangwa ambao unadaiwa kuharibu mashamba ya wakulima.
Ombi hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bagamoyo ,Abdul Sharifu katika baraza la madiwani Halmashauri ya Chalinze.
Katika kikao hicho ilielezwa, tembo wamekithiri na askari waliopo hawatoshelezi kuwadhibiti jambo ambalo linawasababishia wananchi kuendelea kupata hasara ya mazao .
Pia suala la kulipwa fidia likiendelea kuwa kizungumkuti.
Vilevile Sharif alifafanua, idara yoyote ambayo itakuwa sababu kwa Chama hicho kukosa kura kwenye chaguzi zijazo Mkuu wa Wilaya atatakiwa kuichukulia hatua za kinidhamu.
Alieleza, kila mtumishi akisimamia nafasi yake miradi ya maendeleo itakamilika bila vikwazo na kero za wananchi zitapungua.
“Kwa watumishi ambao hawatekelezi wajibu wao ipasavyo wanasababisha wananchi kutupia lawama CCM jambo ambalo hawakubaliani nalo .”
Akizungumzia kuhusiana na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) aliwataka kusimamia kwa ukaribu Wakandarasi wanaowapa kazi ili ziweze kukamilika kwa ubora unaotakiwa.
Alisema baadhi ya Barabara zilizojengwa ikifika kipindi cha mvua zinaharibika na hivyo kero kurejea kwa wananchi.
Sharifu alitoa maelekezo hayo kwa TARURA baada ya Diwani wa Vigwaza Mussa Gama kuelezea kero ya barabara ya Ruvu Darajani-Milo ambayo madaraja matatu yamekuwa kero hasa katika kipindi hiki cha mvua na kushindwa kupitika kwa urahisi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Okash aliahidi kufanyia kazi suala hilo kwa haraka ili kuwanusuru wananchi wanapata kero hiyo.
Hata hivyo alieleza, kitendo cha baadhi ya watumishi kuendelea kukaa ofisini pekee bila kwenda kwa Wananchi ni moja ya sababu zinazochangia kuzorota kwa utekelezaji wa maagizo ya viongozi wa juu.
“Sio wakati wa watendaji kukaa ofisini wakati wananchi wanawahitaji kuwatatulia kero zao.”
“Tukumbuke Rais wetu Samia Suluhu Hassan anatoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali haitapendeza akisikia kuna jambo halisimamiwi vizuri, napenda tufanye kazi kwa ushirikiano tumsaidie Rais kama alivyotuamini” anasisitiza Okash.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze Hassan Mwinyikondo aliielekeza, Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira kuhakikisha wanawaelezea wananchi kuhusiana na utekelezaji wa agizo la Rais Samia la kuwasambazia maji wananchi .
Agizo hilo lilitolewa na Rais Samia Suluhu Hassan aliposhiriki maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Maji yaliyofanyika Mkoani Pwani mwaka 2022 ambapo aliahidi kuipatia DAWASA sh. Milioni 500 kwa ajili ya kazi ya usambazaji wa maji.