NA VERONICA SIMBA,WMA,DODOMA
MEI 13,2026 Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA),Alban Kihulla aliwaambia Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa WMA hufanya uhakiki wa mitungi ya gesi ya kupikia inayouzwa nchini ili kujiridhisha kuhusu ujazo wake kabla ya kuingia sokoni.
Kihulla anayasema haya kwenyw semina kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, kuhusu majukumu ya Wizara ya Viwanda na Biashara na Taasisi zake iliyofanyika bungeni Dodoma.
Kihulla anasisitiza kuwa jukumu la WMA ni kuhakiki na kusimamia usahihi wa vipimo katika sekta zote, ikiwemo nishati.
Hata hivyo anawahimiza wananchi wakiwemo Wabunge kuchukua tahadhari zaidi wakati wa kununua gesi.
“Kabla ya kununua gesi, hakikisheni mtungi huo unapimwa na muuzaji mbele yenu ili kujiridhisha kuhusu ujazo wake. Epukeni kununua gesi kutoka kwa wauzaji wasio na mizani, kwa sababu hutaweza kujua kama gesi uliyonunua ina ujazo sahihi kama ilivyoandikwa kwenye mtungi”, anasema Kihulla.
Akitoa mwongozo wa jinsi ya kutofautisha uzito ulioandikwa kwenye mtungi, Kihulla anaeleza kuwa kila mtungi wa gesi una maelezo mawili muhimu ya uzito ambayo mwananchi anapaswa kuyafahamu ambayo ni Net Weight na Gross Weight.
“Net Weight ni uzito wa gesi pekee iliyomo ndani ya mtungi. Hii ndiyo kiasi unacholipa. Gross Weight ni uzito wa gesi pamoja na uzito wa mtungi tupu.”
Anasema wakati muuzaji anapima mtungi uliojaa gesi, mnunuzi anapaswa kuangalia kama uzito unaooneshwa kwenye mzani unalingana na jumla ya net weight iliyoandikwa kwenye mtungi pamoja na uzito wa mtungi tupu. Ikiwa mzani unaonesha chini ya jumla hiyo, basi kuna upungufu wa gesi.
Anaeleza kuwa changamoto iliyopo kwa sasa ni kuwa wananchi wengi bado hununua gesi kwa mazoea bila kujali kama muuzaji ana mzani na amepima mtungi huo au la.
Anabainisha kuwa baadhi ya wananchi huagiza vijana wa bodaboda kuwanunulia gesi ili kurahisisha usafirishaji, bila wao wenyewe kuwepo ili kujiridhisha. Hali hiyo inawafanya kukosa uhakika kuhusu ujazo halisi wa gesi wanayonunua.
Katika ufafanuzi wake, Kihulla pia anazungumzia upimaji wa tochi za barabarani zinazotumiwa na askari kupima mwendo wa magari.
Anajinasibh kuwa, WMA huhakiki tochi hizo ili kuhakikisha zinapima kwa usahihi na haki inatendeka kwa wamiliki wa magari.
“Hata hivyo, nawasihi wananchi kuwa endapo mtatilia shaka au kubaini kuna tatizo la usahihi wa vipimo popote pale, msisite kuwasiliana na WMA kwa hatua za haraka,” anasema.
Awali, kupitia wasilisho la video, Kihulla anaeleza kuwa WMA inasimamia matumizi sahihi ya vipimo katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, kilimo, miundombinu, madini, maji, ujenzi, nishati na usafiri.
Aidha, anaaema Wakala inajiandaa kuanza uhakiki wa vipimo katika maeneo mapya ikiwemo sekta ya mawasiliano hususan kuhakiki usahihi wa bando za intaneti na dakika za simu zinazotolewa na makampuni ya mawasiliano ili kuongeza wigo wa ulinzi wa mwananchi.
Anahutumisha kwa kusema lengo ni kuhakikisha mteja anapata kiasi halisi cha data au dakika alichonunua, bila kupunguzwa au kupotea kabla ya muda wake kuisha.







