NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua za Vuli (Oktoba – Desemba) 2026, ikitoa angalizo la msimu huo kuathiriwa kwa kiwango kikubwa na hali ya El Niño yenye nguvu kubwa iliyotokana na joto la bahari kuwa Juu ya Wastani katika Bahari ya Pasifiki, hali itakayochagiza ongezeko la Mvua za Vuli 2026 kuwa za Juu ya Wastani hadi Wastani katika maeneo mengi ya Ukanda wa Pwani ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Ukanda wa Ziwa Victoria na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.
Akizungumza juu ya utabiri huo, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabia Nchi (IPCC), Dk.Ladislaus Chang’a alisema:-
“Msimu wa mvua za Vuli 2026 unatarajiwa kuathiriwa kwa kiwango kikubwa na hali ya El Niño yenye nguvu kubwa, hivyo mvua za Juu ya Wastani hadi Wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi Ukanda wa Pwani ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Ukanda wa Ziwa Viktoria na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma”. aliongezea kusema kuwa Mvua hizo zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Septemba hadi wiki ya kwanza ya mwezi Oktoba 2026 katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Viktoria, na kusambaa taratibu katika maeneo mengine katika mwezi Oktoba 2026.
Aidha alifanunua kuwa kwa kawaida mvua za Vuli huisha mwezi Desemba japo katika msimu wa Vuli 2026 mvua za nje ya msimu zinatarajiwa kuendelea hadi mwezi Januari 2027, na ongezeko la mvua likitarajiwa hasa katika kipindi cha mwezi Novemba 2026.
Akielezea juu ya athari zinazotarajiwa, Dk.Chang’a ametahadharisha kuwa “vipindi vya unyevu kwenye udongo wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo,” pia aliongezea kusema kuwa ongezeko la kina cha maji katika mabwawa na mito linaweza kuathiri miundombinu ya rasilimali za maji na nishati, huku magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza kutokana na uchafuzi wa maji. Magonjwa ya mazao yanayosababishwa na kuvu, bakteria na virusi yanaweza kuathiri uzalishaji wa viazi mviringo, alizeti, maharage, ufuta pamoja na matunda na mbogamboga, huku sekta za usafiri, ujenzi na utalii zikitarajiwa kukumbwa na changamoto za mmomonyoko wa barabara, uharibifu wa madaraja na kuhama kwa wanyamapori kutokana na mafuriko.
Katika hitimisho lake, Dk. Chang’a amewashauri Wadau wa sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii kupanga na kutekeleza shughuli zao kwa kuzingatia taarifa mahususi za hali ya hewa zinazotolewa na TMA ikiwa ni pamoja na kuvuna maji ya mvua, kuimarisha miundombinu, kutoa tahadhari za mapema na kudhibiti mazalia ya mbu ili kupunguza magonjwa ya mlipuko.

