NA MWANDISHI WETU,MOROGORO
KATIBU Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dk.Jim Yonazi, ametoa wito kwa wananchi kutumia Vituo vya Maarifa ili kupata huduma mbalimbali za afya na kufahamu hali zao za kiafya, hususan kuhusu maambukizi ya VVU na UKIMWI.
Dk. Yonazi ametoa wito huo leo Mei 19, 2026, wakati wa ziara ya kukagua utendaji wa Vituo vya Maarifa vya Dumila mkoani Morogoro na Kibaigwa mkoani Dodoma.
Akizungumza baada ya kutembelea vituo hivyo, Dk. Yonazi alisema Serikali itaendelea kuimarisha na kusambaza Vituo vya Maarifa katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha wananchi wengi wanapata huduma za ushauri nasaha, elimu ya afya na upimaji bila malipo.
“Nitoe wito kwa wananchi wetu kuendelea kutumia Vituo vya Maarifa kwa wingi ili waweze kupata ushauri, huduma na elimu mbalimbali ya afya, hususan kuhusu maambukizi ya Virusi vya UKIMWI. Serikali itaendelea kuweka vituo hivi kote nchini,” alisema Dk. Yonazi.
Aidha, alisema Serikali ina mpango wa kukutana na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kwa lengo la kuweka utaratibu utakaowezesha Vituo vya Maarifa kuendeshwa katika ngazi ya halmashauri, hatua itakayosaidia huduma hizo kuwafikia wananchi kwa ufanisi zaidi.
Alifafanua kuwa utaratibu huo mpya utalenga kuongeza ushiriki wa mamlaka za serikali za mitaa katika uendeshaji wa vituo hivyo badala ya kutegemea usimamizi wa Serikali Kuu pekee kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS).
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dk. Adam Mrisho, amesema taasisi hiyo itatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Katibu Mkuu na kushughulikia changamoto zote zilizobainika wakati wa ziara hiyo.
Dk. Mrisho alisisitiza kuwa TACAIDS itaendelea kuboresha utoaji wa huduma za kinga, elimu na ushauri kuhusu VVU na UKIMWI ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati.








