NA EDNA BONDO,MOROGORO
WAZIRI wa Madini,Anthony Mavunde, amesema ndani ya kipindi cha Miaka Minne, (4) Sekta ya Madini imevutia uwekezaji wa Sh.Trilioni 9, hatua inayoiweka Tanzania kuwa kivutio cha uwekezaji wa Madini Barani Afrika.
Amesema hayo leo Jumamosi Agosti 15, 2026, mkoani hapa wakati wa hafla ya utiaji saini wa Mikataba ya Ubia wa Uchimbaji wa Madini ya Kinywe baina ya Serikali na Kampuni ya Henan Yudi Mining na kuongeza kuwa, hadi sasa tayari jumla ya mikataba ya Msingi 14 imekwisha sainiwa.
Amesema kuwa mradi huo una mashapo yaliyothibitishwa ya takribani tani milioni 104.28 za kinywe, na unatarajiwa kuwekeza takribani Dola milioni 100 (Shilingi bilioni 265) huku uzalishaji wa kiwango kamili ukilenga kufikia tani 50,000 za kinywe kwa mwaka na kwamba mradi unatakuwa na uwezo wa kuchakata tani milioni moja kwa mwaka wakati huohuo zaidi ya Watanzania 600 wakitarajiwa kupata ajira za moja kwa moja.
Mavunde amesema Serikali inaendelea kuimarisha nafasi yake katika sekta ya madini kutoka kuwa mwenyeji wa uchimbaji hadi kuwa mshiriki wa thamani inayozalishwa, ambapo katika mradi huo Serikali inamiliki asilimia 17 ya hisa.
Amesema kinywe ni madini muhimu katika teknolojia za kisasa, ikiwemo utengenezaji wa anode za betri, hivyo mradi huo una nafasi ya kuchangia katika azma ya Tanzania kushiriki zaidi kwenye mnyororo wa thamani wa kinywe duniani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, amesema Serikali ya Wilaya inashukuru juhudi zilizofanyika kufanikisha makubaliano hayo, akieleza kuwa mradi unatarajiwa kufungua fursa za kiuchumi na ajira, kuongeza uzalishaji wa madini na kuchochea maendeleo ya sekta ya madini na uchumi wa Taifa.
Aidha, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, amezipongeza pande zote zilizoshiriki katika majadiliano hayo, akisema mradi huo utaongeza uwekezaji wa kibiashara nchini, kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na China.
Balozi Chen amesema China ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa uwekezaji wa moja kwa moja nchini Tanzania, huku akieleza kuwa mradi huo unaongeza eneo jingine la ushirikiano wa kibiashara kati ya mataifa hayo na kufungua fursa za ajira na maendeleo ya kiuchumi kwa eneo la mradi na Taifa kwa ujumla.










