NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
WADAU wa Michezo hapa nchini wamehimizwa kutumia huduma za Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kusajili kazi zao za ubunifu.
Aidha wametakiwa kujifunza kuhusu haki zao ili kuleta tija na ufanisi ili kuwakomboa kiuchumi.
Rai hiyo imetolewa Mei 08, 2026 na Waziri wa Viwanda na Biashara Judith Kapinga katika maadhimisho ya siku ya Miliki Ubunifu Duniani yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam.
Kapinga alisema kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha wanamichezo na wadau wa sekta hiyo wanatumia Miliki Ubunifu kukuza tasnia ya michezo hapa nchini.
“Niwasihi viongozi wa vilabu vya michezo, mashirikisho na wadau wote wa michezo kuwasaidia wanamichezo katika vilabu na mashirikisho yenu kuhakikisha wanalinda haki zao ikiwemo matumizi ya picha au taswira zao katika bidhaa au biashara za watu wengine,’’ alisema Kapinga.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa aliwakumbusha wadau na wanamichezo kutumia majina yao vizuri ‘Brand Names’ kujiandaa na maisha mengine baada ya kustaafu michezo.
“Naomba nitoe mifano michache kwa wachezaji wa kimataifa wanaoendelea kunufaika kwa kutumia Alama za Biashara ingawa wengine wameshajiuzulu michezo, Alama ya biashara (logo) ya CR7 inayomilikiwa na mchezaji wa mpira wa miguu Christiano Ronaldo ni Dola za Kimarekani Milioni 900,” alisema Nyaisa
Kwa upande wake ,Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa BRELA Prof. Neema Mori alisema ni muhimu wadau wa michezo wakajiepusha kabisa kutumia Miliki Ubunifu kama vile Alama za biashara (logo) zisizo zao pasipo idhini ya wamiliki halisi ili kuepuka kuingia katika matatizo ya kisheria kwa kutumia Alama zilizosajiliwa na watu wengine.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) Mhandisi Leodgar Tenga alisema wakati Taifa likiwa kwenye maandalizi ya AFCON 2027 ni vyema wafanyabiashara na wadau wote wa michezo wakahakikisha wamelinda bunifu zao ili kuepuka wizi na uharamia kwenye bidhaa na huduma kwa upande wa matumizi ya Alama (brands) zilizopata umaarufu na ambazo ni bora.
Maadhimisho ya Miliki Ubunifu na Utoaji wa Tuzo za Miliki Ubunifu kwa wadau wa michezo mwaka huu yamefanyika yakiwa na kauli mbiu isemayo “Miliki Ubunifu na Michezo; Jitayarishe, Jipange, Vumbua.”
Sambamba na maadhimisho hayo ,Brela ilitoa Tuzo mbalimbali ikiwemo Mwandishi bora wa Habari za michezo ambapo Prisca Kishamba wa Kituo cha Clouds Media group aliibuka kuwa mshindi huku Azam Media ikiibuka na Tuzo ya kufanya vizuri katika kutangaza na kuonesha mechi za mpira wa miguu hapa nchini.
Mwingine ni Rehema Selemani Mwanamichezo Mlemavu mwenye mchango mkubwa wa mabadiliko kwenye sekta ya michezo nchini.
Aidha Timu za Yanga,Simba na Azam pia zilitunukiwa Tuzo za kufanya vizuri katika michuano mbalimbali ya Ligi.
Tuzo ya Mkimbiaji bora ya Kimataifa ilikwenda kwa Alphonce Simbu.
Kwa upande wa Taasisi za Fedha zilizofanya vizuri kwenye udhamini katika Michezo na kupewa Tuzo ni benki ya NBC na CRDB.
Wakati huo huo Mjasiriamali wa kuzalisha mvinyo na keki Mwilongo Mapembe Semapembe alipata Tuzo ya mjasiriamali bora kwa kike aliyesajili jina na matumizi mazuri ya alama za biashara kwenye bidhaa anazozalisha










