NA MWANDISHI WETU,DJIBOUTI
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Thabit Kombo amemuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan katika sherehe za uapisho wa Rais wa Jamhuri ya Djibouti Ismaïl Omar Guelleh, zilizofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Djibouti uliopo jijini hapa
Pia Waziri Kombo amewasilisha Ujumbe Maalumu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan kwa Rais wa Jamhuri ya Djibouti Ismaïl Omar Guelleh.
Rais Guelleh amechaguliwa kuongoza nchi hiyo kwa muhula wa sita mfululizo kufuatia ushindi alioupata kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Aprili 10, 2026.
Rais Guelleh mwenye umri wa miaka 78, amehudumu katika nafasi hiyo kwa miaka 27 sasa akiliongoza taifa hilo dogo la Pembe ya Afrika lenye watu takribani milioni moja.
Aidha, Waziri Kombo baada ya sherehe za uapisho alimkabidhi Rais Guelleh ujumbe maalumu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan.
Sherehe hizo za uapisho zimehudhuriwa na Wakuu wa nchi mbalimbali kutoka Ethiopia, Somalia, Sudan Kusini, Gabon na Yemen, pamoja na viongozi wengine mbalimbali waliowawakilisha wakuu wa nchi zao.
Akihutubia baada ya kuapishwa, Rais Guelleh amewashukuru wananchi wa Djibout kwa imani na heshima kubwa waliyompatia na akaahidi kuboresha mifumo ya Elimu, kukuza uchumi na teknolojia, kuimarisha usalama wa kikanda na kuongeza ajira.
Akizungumza baada ya sherehe hizo, Waziri Kombo amempongeza Rais Guelleh kwa ushindi aliopata na kumtakia heri katika kuwatumikia wananchi wa Djibouti ambao wameonyesha imani kubwa kwake.
Aidha Kombo amesema Tanzania na Djibouti ni nchi marafiki wa muda mrefu wenye uhusiano mzuri na kutoa rai kwa wananchi wa Tanzania na Djibouti kuhakikisha wanauendeleza urafiki huo kwa manufaa wa wananchi wa pande zote mbili.








