NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dk.Aneth Komba leo Ijumaa Machi 27,2026 amefunga rasmi kikaokazi cha siku tatu cha kuandaa maudhui ya Kuhesabu katika “Kalimani App” kwa kutumia Mtaala ulioboreshwa wa Mwaka 2023 na Kamusi ya Lugha ya Alama ya Tanzania jijini Dar ES salaam.
App hiyo inaandaliwa kwa ajili wanafunzi viziwi wa Darasa la Awali, la Kwanza na la Pili.
Akifunga kikao kazi hicho Mkurugenzi Mkuu Dk. Komba amesema, maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 yemejikita katika kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa ni jumuishi na kuwa hakuna mtoto hata mmoja anayeachwa.
“Wazazi wenye watoto wenye mahitaji maaalum naomba muwapeleka shuleni kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeandaa mazingira wezeshi kwa watoto wote wakiwemo wenye mahitaji maalumu.”amesema Dk.Komba
Pia , amewashukuru Jenga Hub kwa maono na ubunifu wao katika kuandaa App hii ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Kisayansi wa KKK, uliozinduliwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan hivi karibuni.
Vilevile, ameeleza kuwa TET itashirikiana kwa ukaribu na Jenga Hub kuhakikisha kuwa lengo la kuandaa App linafikiwa na kuwa App hii inawanufaisha walengwa wote nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Jenga Hub iliyobuni Kalimani App,Nancy Sumari, ameeleza kuwa App hii imelenga kutumiwa na watoto viziwi wa Darasa la Awali, Darasa la Kwanza, Pili na la Tatu.
Aidha, ameeleza kuwa Kalimani App inaandaliwa kwa ushirikiano kati ya Jenga Hub na TET na kuwa itawawawezesha watoto viziwi kujifunza Kuhesabu kwa urahisi na hivyo kuhakikisha lengo la serikali la kuwawezesha wanafunzi kuweza kuhesabu kwa ufasaha kabla ya kufika Darasa la Tatu linafikiwa.
Hata hivyo Sumari ameishukuru sana TET kwa kuwa tayari kushirikiana na taasisi ya Jenga Hub katika kuhakikisha kuwa watoto viziwi nao wanapata haki yao ya msingi ya kupata vifaa vya kufundishia na kujifunzia.











