NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
MKUU wa Chuo cha Ulinzi wa Amani Tanzania (TPTC), Brigedia Jenerali George Itang’are amesema suala la afya ya akili kwa wanajeshi wanaokwenda katika misheni za kulinda amani ni jambo muhimu linalopaswa kupewa uzito mkubwa kutokana na mazingira magumu wanayokutana nayo wakiwa kazini.
Brigedia Jenerali Itang’are ameyasema hayo leo Mei 18,2026 jijini Dar es Salaam wakati akifungua kozi mbili maalum chuoni huku moja ya kozi hizo inalenga kuwaandaa wakufunzi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) watakaokuwa na jukumu la kuwafundisha walinzi wa amani kuhusu afya ya akili kabla ya kupelekwa kwenye misheni mbalimbali za kimataifa.
Amesema wanajeshi wanaofanya kazi za ulinzi wa amani hukutana na changamoto nyingi zinazoweza kusababisha msongo wa mawazo, hofu na athari nyingine za kisaikolojia, hivyo maandalizi ya afya ya akili kabla ya kuondoka ni muhimu kwa usalama na utendaji wao.
“Ni muhimu walinzi wa amani wakafahamu mapema mazingira watakayokutana nayo wanapokwenda misheni, lakini pia wajue namna ya kukabiliana na changamoto za kisaikolojia wanazoweza kupitia,” amesema Brigedia Jenerali Itang’are.
Amefafanua kuwa kozi hiyo ya wakufunzi inalenga kuhakikisha walinzi wa amani wanakuwa katika hali nzuri ya afya ya akili kabla ya kuondoka nchini, pamoja na kuweka mfumo wa kuwafuatilia hata wanapokuwa wamerejea kutoka misheni.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa chuo, mafunzo hayo yanafanyika kwa mara ya kwanza kabla ya kuanza kwa mzunguko mpya wa mafunzo kwa walinzi wa amani watakaokwenda katika misheni za kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Aidha, Brigedia Jenerali Itang’are alisema kozi ya pili inayotolewa chuoni hapo inawahusu wakufunzi wa sekta ya tiba katika shughuli za ulinzi wa amani. Alisema mafunzo hayo yamewakutanisha wataalamu kutoka nchi mbalimbali kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu bora za utoaji huduma za afya kwa walinzi wa amani.
Alisisitiza kuwa kozi hizo pia zinawawezesha washiriki kupata leseni maalum ya kutibu walinzi wa amani katika misheni za kimataifa, akibainisha kuwa bila leseni hiyo hakuna mtu anayeruhusiwa kushiriki katika misheni hizo za ulinzi wa amani.
Naye Mkufunzi Mkuu wa afya ya akili TPTC, Dk. Annie Lasway amesema mafunzo na uhamasishaji kuhusu afya ya akili ni sehemu muhimu katika kuhakikisha wanajeshi pamoja na watumishi wa afya wanakuwa salama kiakili na wenye uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Amesema tatizo la afya ya akili ni kubwa, hasa katika sekta ya kijeshi, ambapo takribani asilimia 72 ya watu huhitaji kiwango fulani cha huduma ya afya ya akili.
Hata hivyo, ameeleza kuwa hali hiyo si tofauti sana na ilivyo katika jamii kwa ujumla, kwani changamoto nyingi zinachangiwa na uelewa mdogo wa masuala ya afya ya akili pamoja na ukosefu wa uvumilivu na kukubalika kwa watu wenye changamoto hizo.
Aidha, Dk. Lasway ameonya kuwa iwapo wanajeshi hawatapatiwa msaada unaohitajika, madhara yanaweza kuwa makubwa zaidi, sawa na ilivyo kwa matatizo mengine ya kiafya yanapoachwa bila kushughulikiwa.
“Tatizo lolote lisipopatiwa ufumbuzi linaweza kuongezeka na kuwa baya zaidi, hali ambayo inaweza kuathiri kazi zao, majukumu yao ndani ya jamii pamoja na maisha yao kwa ujumla,” amesema.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu na msaada wa kitaalamu ili kuhakikisha wanajeshi pamoja na watumishi wa afya wanapata mazingira salama ya kuzungumzia changamoto za afya ya akili bila hofu wala unyanyapaa.





