NA MWANDISHI WETU, RORYA,MARA
MAMLAKA ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imetangaza fursa ya mafunzo ya mbolea kwa wakulima na wananchi wanaotamani kuanzisha biashara ya mbolea katika vijiji vya Tatwe, Nyamusi na Panyakoo vilivyopo Wilaya ya Rorya, mkoani Mara.
Akizungumza Desemba 11, 2025, akitekeleza kampeni ya ‘Mali Shambani’, Ofisa Udhibiti Ubora Mwandamizi kutoka TFRA, Godwin Vedastus, alisema kuwa elimu hiyo ya mbolea inatolewa bure ikilenga kuongeza mawakala wa mbolea na hivyo kuwahakikishia wakulima upatikanaji wa mbolea karibu na makazi yao.
“Mamlaka inatoa mafunzo haya bure ili kumsaidia mkulima apate mbolea kwa urahisi. Mtu yeyote anayehitaji kuingia katika biashara ya mbolea anakaribishwa kupata leseni bila gharama,” alisema Vedastus.
Kwa upande wake, Ofisa Masoko kutoka Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), Shafi Omary, alisema kuwa kampuni hiyo imepunguza masharti ya usajili kwa mawakala wapya ambapo inasajili mawakala kwa kianzio cha mifuko 20 pekee lengo likiwa ni kupanua mtandao wa usambazaji wa mbolea nchini.
Naye Ofisa Mawasiliano na Masoko wa Minjingu Fertilizers Ltd, Kisuma Mapunda, alisisitiza kuwa, kampuni hiyo pia imerahisisha masharti kwa wakulima na vijana wanaotaka kuingia katika biashara ya mbolea.
“Kwa Minjingu, mtu anaweza kuwa wakala kwa kianzio cha kuanzia shilingi 500,000 tu. Tumepunguza gharama ili kuwapa nafasi wakulima na vijana kujiendeleza kiuchumi,” alisema Mapunda.
Kupitia fursa hizi, wakulima wa Rorya wanatarajiwa kunufaika na upatikanaji wa mbolea kwa urahisi zaidi, huku vijana na Wajasiriamali wakifunguliwa milango ya kujiendeleza kiuchumi.
Hatua hii inatarajiwa kuongeza idadi ya Mawakala na kuboresha mnyororo mzima wa usambazaji wa pembejeo za kilimo katika mkoa wa Mara.



