NA MWANDISHI WETU,KILIMANJARO
MAMLAKA ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imewahakikishia wakulima wa kanda ya kaskazini kuwa mbolea zipo za kutosha kwa ajili ya msimu wa kilimo unaoendelea, huku jitihada za usambazaji zikiendelea kuimarishwa ili kuhakikisha pembejeo hiyo muhimu inawafikia wakulima kwa wakati.
Uhakika huo umetolewa kufuatia ziara ya maafisa wa TFRA katika maghala ya kampuni za mbolea jijini Dar es Salaam anbako ndio kwenye chanzo kikubwa cha mbolea kwa lengo la kujionea hali ya upatikanaji wa mbolea pamoja na mipango ya usambazaji wake katika maeneo mbalimbali hususan kanda ya Kaskazini.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwakilishi wa kampuni ya ETG Inputs Limited, Rakesh Patel, amesema kampuni hiyo ina akiba ya kutosha ya mbolea kwa ajili ya msimu huu wa kilimo unaoelekea kumalizika yaani 2025/2026.
“Tunazo mbolea za kutosha kukidhi mahitaji ya wakulima tunaowahudumia kwa msimu huu wa kilimo unaoendelea.
“Tayari usafirishaji unaendelea kuelekea katika mikoa ya kanda ya kaskazini ikiwemo Arusha, Kilimanjaro na Tanga,” amesema Patel.
Ameongeza kuwa lori lenye uwezo wa kubeba tani 30 za mbolea tayari limepakia na linaelekea katika mikoa hiyo ili kuhakikisha mbolea zinawafikia wasambazaji na hatimaye wakulima kwa wakati.
Aidha, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji (TFRA) Meneja wa Tehama Robert Mtendamema amesema TFRA inaendelea kufanya ufuatiliaji wa karibu wa upatikanaji na usambazaji wa mbolea nchini ili kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo hiyo muhimu kwa wakati na kwa bei inayowekwa na Mamlaka.
Mtendamema amesema zoezi la kutembelea na kukagua maghala linaendelea katika mikoa ya Dar es salaam na Kilimanjaro
ili kujiridhisha na uwepo wa mbolea tayari kwa kuwahudumia wakulima.
Vilevile akithibitisha upatikanaji wa mbolea mapema leo Meneja (TFRA) Kanda ya Kaskazini Bw. Gothard Liampawe amesema hali ya upatikanaji wa mbolea katika mkoa wa kilimanjaro unaendelea kuimarika ambapo jumla ya tani 118.5 za mbolea za kukuzia zimeuzwa na kusambazwa kwa wakulima katika Wilaya ya Moshi, Hai na Siha.
Aidha amesema jitihada zinaendelea kufanyika na Mamlaka ambapo kesho tarehe 17.04. 2026 tani 153.5 zitaendelea kuuzwa katika vituo mbalimbali vya usambazaji katika wilaya hizo.
Liampawe amesema kuwa ongezeko la matumizi ya mbolea kwa wakulima katika kanda hiyo umetokana na kuongezeka kwa watumiaji wa mbolea baada ya kampeni ya matumizi sahihi ya mbolea ya Mali Shambani,iliyofanyika kuanzia mwezi Oktoba 2025 hadi Machi 2026 na hivyo kuleta mwamko mkubwa kwa wakulima kutumia mbolea.







