NA MWANDISHI WETU,KILIMANJARO
WAKULIMA Kanda ya Kaskazini, hususan mkoa wa Kilimanjaro wamehakikishiwa upatikanaji wa mbolea ya kutosha kwa msimu huu wa kilimo, hali inayoashiria kuimarika kwa sekta hiyo muhimu ya uzalishaji wa chakula.
Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) Kanda ya Kaskazini, Gothard Liampawe, amesema hayo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, akibainisha kuwa hali ya upatikanaji wa mbolea kwa sasa ni ya kuridhisha na imeboreshwa kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na vipindi vilivyopita.
Amesema TFRA kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya kilimo wameweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha mbolea inasambazwa kwa wakati, inapatikana kwa wingi na kwa bei nafuu ili kuwasaidia wakulima kuongeza tija katika uzalishaji.
“Kwa sasa hakuna uhaba wa mbolea. Ipo ya kutosha katika maeneo mbalimbali ya Kanda ya Kaskazini, na wakulima wanahimizwa kuitumia ipasavyo ili kuongeza mavuno,” alisema Liampawe.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa wakulima kununua mbolea kutoka kwa wauzaji waliothibitishwa ili kuepuka bidhaa zisizo na ubora, pamoja na kufuata maelekezo ya wataalamu wa kilimo kuhusu matumizi sahihi ya pembejeo hizo.
Sambamba na hilo, Liampawe ametoa onyo kali kwa Mawakala na wasambazaji wa mbolea wanaokiuka taratibu, akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayehusika na uuzaji wa mbolea feki, kupandisha bei kiholela au kuhujumu upatikanaji wa pembejeo hiyo muhimu.
Amesema TFRA itaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa wauzaji na maghala ya mbolea ili kuhakikisha wanazingatia viwango vilivyowekwa, huku akiwataka wakulima kutoa taarifa kwa mamlaka husika pale wanapobaini vitendo vya udanganyifu.
Pamoja na mambo mengine,
-
juhudi za serikali kupitia TFRA pamoja na ushirikiano wa wadau zimeleta mafanikio chanya, hali inayotoa matumaini kwa wakulima wa Kanda ya Kaskazini kupata mavuno bora katika msimu huu wa kilimo.






