NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeimarisha uwezo wake wa kifedha na kufikia Sh.Trilioni 1.31/-huku kupitia programu ya MEFI, mfuko huo umetoa mikopo ya Sh. Bilioni 51.15 kwa vituo 493 vya afya tangu mwaka 2007 na Sh.Bilioni 129.2 zikitumika katika Hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa kwa ajili ya kuboresha huduma za kibingwa.
Akizungumza katika kikao kazi kati ya NHIF na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina leo Novemba 6, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dk. Irene Isaka amesema kiasi hicho kilichofikiwa mwishoni mwa mwaka wa fedha 2025/26 kinauwezesha mfuko huo kutekeleza majukumu yake kwa zaidi ya miaka miwili.
Dk. Isaka amesema katika mwaka wa fedha 2024/25, mapato ya bima yaliongezeka hadi Sh bilioni 773.42 kutoka Sh bilioni 700.11 mwaka uliotangulia, huku gharama za huduma za bima zikipungua kwa asilimia 10.
Katika kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za matibabu, NHIF imeendelea kutoa mikopo kwa vituo vya afya kwa ajili ya kuboresha miundombinu, kununua vifaa tiba na kuimarisha huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Aidha, amesema NHIF imeendelea na utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, ambapo kuanzia Februari 2026 ilianza zoezi la uhakiki na utoaji wa kadi za bima kwa kaya zisizo na uwezo.
“Katika mpango huo, Serikali imelipa Sh.bilioni 41.4 kwa ajili ya kaya 276,000 zenye wanufaika 1,206,319 katika mikoa yote ya Tanzania Bara,” amesema Dk. Isaka
Hata hivyo, amesema takwimu za mfuko zinaonesha kuwa hadi wakati wa tathmini, kaya 198,709 kati ya 276,004 zilizolengwa zilikuwa zimepatiwa kadi, sawa na asilimia 72 ya lengo, huku wanufaika 542,829 kati ya 1,206,319 wakipatiwa kadi.
Kwa upande wa makundi maalumu, NHIF imeendelea kutoa kadi za bima kwa wazee na watoto wanaoishi katika makazi na taasisi maalumu, huku ikiandaa utekelezaji wa awamu ya pili ya usajili wa kaya zisizo na uwezo.
Katika kuongeza upatikanaji wa bima kwa wananchi wa sekta rasmi na isiyo rasmi, amesema mfuko umeweka mikakati mbalimbali ikiwemo kufungua ofisi ndogo katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya wananchi, kushirikisha mawakala wa bima na kuimarisha ushirikiano na mabenki, kampuni za simu na vyama vya ushirika.
“Pia, NHIF imeanzisha kifurushi cha bima ya afya kwa makundi kinachowawezesha wananchi kujiunga kupitia vikundi vya kuanzia wanachama 10, kwa mchango wa Sh 60,000 kwa mwaka kwa kila mwanachama,” amesema Dk. Isaka

