NA MWANDISHI WETU,DODOMA
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imeielekeza Wizara ya Madini kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa sheria zinazohusu ufungaji migodi na utunzaji wa mazingira, sambamba na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kuhakikisha kampuni za uchimbaji madini zinatimiza wajibu wake wa kurejesha maeneo ya migodi katika hali salama baada ya shughuli za uchimbaji kukoma.
Maelekezo hayo yametolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo,Mashimba Ndaki, akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa Kamati wakati wa semina kuhusu utaratibu wa kisheria wa ufungaji migodi na uwekaji wa dhamana za urekebishaji iliyofanyika katika Ukumbi wa Tume ya Madini jijini Dodoma.
Ndaki amesema ni muhimu kuhakikisha sheria na kanuni zinazohusu ufungaji migodi zinasimamiwa ipasavyo ili kulinda mazingira, usalama wa wananchi na kuhakikisha maeneo yaliyotumika kwa shughuli za uchimbaji yanarejeshwa katika hali inayokubalika.
Amesisitiza umuhimu wa Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini kuendelea kuimarisha usimamizi wa migodi na kuhakikisha wamiliki wa leseni wanatekeleza matakwa ya kisheria kuhusu uandaaji wa Mipango ya Ufungaji Migodi pamoja na uwekaji wa Dhamana za Urekebishaji.
Aidha,Ndaki ameipongeza Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini kwa hatua zilizopigwa katika kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye uchumi wa Taifa, ambapo kwa sasa sekta hiyo inachangia asilimia 10.3 ya bajeti kuu ya Serikali.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema wamepokea maelekezo ya Kamati na watayafanyia kazi na kuishukuru kamati kupitia wajumbe kwa michango yao mizuri waliyotoa kwa ajili ya kuboresha sekta ya madini.
Amesema serikali inaendelea kuimarisha sekta ya madini kwa kuweka mikakati inayolenga kuongeza uzalishaji, ushiriki wa Watanzania katika shughuli za uchimbaji, upatikanaji wa mitaji na teknolojia pamoja na kuimarisha usimamizi wa migodi na mazingira.
Mavunde pia amesema kwa mwaka tani 67 za dhahabu zimesajiliwa nchini, hatua inayoonesha umuhimu wa sekta hiyo katika kukuza uchumi na kuongeza mapato ya Serikali.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania pamoja na taasisi za fedha katika kuanzisha Mfuko wa Dhamana ya Mikopo kwa Wachimbaji, utakaosaidia kuwawezesha kupata mikopo kwa ajili ya kununua vifaa, teknolojia na kuongeza uzalishaji.
Katika kuongeza mapato ya Serikali, Mhe. Mavunde amesema kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Tume ya Madini imelenga kukusanya Shilingi trilioni 1.4, huku katika kipindi cha Julai hadi Oktoba 2026 ikiwa imekusanya Shilingi bilioni 552.
Amesema Serikali inalenga kuongeza makusanyo hadi kufikia Shilingi bilioni 800 ifikapo Desemba 2026, sambamba na kuanza kwa safari za ndege za utafiti wa madini katika mikoa mbalimbali nchini kuanzia mwezi huo.
Awali, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira wa Tume ya Madini, Mhandisi Hamisi Kamando, akiwasilisha mada katika semina hiyo amesema Tume imeimarisha usimamizi wa ufungaji migodi kwa kuhakikisha wamiliki wa leseni za uchimbaji mkubwa na wa kati wanaandaa na kuwasilisha Mipango ya Ufungaji Migodi kwa ajili ya kufanyiwa mapitio na kuidhinishwa.
Amesema kwa mujibu wa Kanuni ya 206(1) ya Kanuni za Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira za Mwaka 2010, kila mmiliki wa leseni ya uchimbaji mkubwa na wa kati anatakiwa kuandaa na kuwasilisha kwa Mkaguzi Mkuu wa Migodi mpango unaobainisha namna eneo la mgodi litakavyorejeshwa na kurekebishwa baada ya shughuli za uchimbaji kukoma.
Ameongeza kuwa baada ya kupokea mpango huo, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Migodi hufanya mapitio ya awali kabla ya kuitisha kikao cha Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji Migodi (NMCC) kwa ajili ya kujadili na kuamua kuuidhinisha au kutouidhinisha.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 206(3), Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji Migodi inajumuisha wawakilishi kutoka Wizara zinazohusika na madini, mazingira, maji na maliasili, mamlaka za mikoa na wilaya, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na taasisi nyingine husika.
Mhandisi Kamando amesema mpango wa ufungaji mgodi hauishii katika kufunga eneo la uchimbaji pekee, bali unajumuisha urejeshaji wa ardhi na vyanzo vya maji, usalama wa miundombinu ya mgodi, gharama za kulipa stahiki za kisheria za wafanyakazi pamoja na programu za kuwezesha jamii zinazozunguka migodi kuwa na shughuli mbadala za kiuchumi.
Amesema katika kuhakikisha gharama hizo zinapatikana, wamiliki wa migodi wanatakiwa kuweka Dhamana za Urekebishaji ambazo zinaweza kuwa katika mfumo wa akaunti ya Escrow, dhamana ya mtaji, dhamana ya bima au dhamana ya benki.
Kwa mujibu wa takwimu zilizowasilishwa katika semina hiyo, nchini kuna migodi 84 ya uchimbaji mkubwa na wa kati, ambapo migodi 44 imewasilisha Mipango ya Ufungaji Migodi, mipango 36 imejadiliwa na Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji Migodi na mipango 21 imeidhinishwa.
Hata hivyo, ni migodi miwili pekee, North Mara na Bulyanhulu, iliyoweka dhamana za urekebishaji kupitia kampuni ya bima ya MUA Januari 16, 2026.
Serikali inaendelea kusisitiza umuhimu wa usimamizi wa sheria hizo ili kuhakikisha shughuli za uchimbaji madini zinaendana na uhifadhi wa mazingira, usalama wa wananchi na maendeleo endelevu ya jamii zinazozunguka maeneo ya migodi.









