NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umetangaza mpango wa kuwakatia bima ya afya waandishi wa habari 100 kutoka mikoa mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano na vyombo vya habari katika kuhamasisha wananchi kujiunga na bima ya afya.
Mpango huo unatarajiwa kugharimu Sh. Milioni sita na utaanza kutekelezwa mkoani Dodoma, ambako waandishi 30 watapatiwa bima kupitia klabu za waandishi wa habari (Press Clubs).
Hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya Mfuko kuimarisha ushirikiano na wahariri na waandishi wa habari, ambao unaelezwa kuwa muhimu katika kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa bima ya afya na huduma zinazotolewa na NHIF.
Akizungumza katika kikao kazi kati ya NHIF na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina leo Ijumaa Novemba 6, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dk. Irene Isaka amesema kuwa vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kujenga uelewa wa wananchi, kuondoa dhana potofu na kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu bima ya afya.
Aidha amesema NHIF imeandaa mbio ambazo zitashirikisha watumishi, wageni waalikwa na wananchi 10,000 kwa lengo la kuhamamisha afya, kuzuia magonjwa yasiyo ya kuambukiza na kuchangia kutoa kadi za bima za mwaka mzima kwa makundi maalum.
Katika kuendeleza ushirikiano huo wa NHIF na vyombo vya habari, Dk.Isaka amesema mfuko huo utahharamia viingilio vya waandishi 135 watakaoshiriki mbio hizo zinazolenga kuhamasisha wananchi kujali afya zao, kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza pamoja na kuchangia jamii.
“NHIF itawalipia waandishi hao viingilio vya mbio ili wawe Mabalozi wazuri katika kuelimisha umma umuhimu wa bima ya afya na kujikinga na magonjwa yasiyoambukizwa, Dodoma tutachukua waandishi 40 kupitia Press Club zao,” amesema Dk. Isaka
Kikao hicho pia kilitumika kueleza mafanikio ya Mfuko huo katika kipindi cha miaka 25 tangu kuanzishwa kwake, ikiwemo ukuaji wa wanachama, uimarishaji wa uwezo wa kifedha, matumizi ya teknolojia na hatua mbalimbali za utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.
Kwa mujibu wa Dk.Isaka, mfuko ulianza rasmi Julai 1, 2001, ukiwahudumia watumishi wa Serikali Kuu pekee, lakini umeendelea kupanua wigo wa huduma zake kwa makundi mbalimbali ya wananchi.
Amesema kuwa idadi ya wanufaika imeongezeka kutoka 691,773 wakati wa kuanza kwake hadi 7,109,771 katika mwaka wa fedha 2025/26, sawa na asilimia 10.5 ya Watanzania.
“Ukuaji huu umehusishwa na maboresho ya huduma, urahisishaji wa usajili kupitia mifumo ya kidijitali pamoja na kuingizwa kwa makundi mapya ya wanufaika,” amesema Dk. Isaka











