NA FLORAH AMON, DAR ES SALAAM

JUMLA ya Dola za Marekani Milioni 49.5, sawa na takriban Sh.Bilioni 121 za Kitanzania, zimetolewa na Benki ya Dunia kwa ajili ya kuboresha miundombinu, mitaala na ubora wa elimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Uchumi (HEET).

Fedha hizo ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa Mradi wa HEET wenye thamani ya Dola Milioni 425, unaotekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Akizungumza katika mkutano uliowakutanisha Wahariri pamoja na na Waandishi wa habari uliofanyika chuoni hapo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye, amesema mradi wa HEET ni zaidi ya ujenzi wa majengo, kwani unalenga kuleta mageuzi makubwa katika mfumo wa elimu ya juu nchini.

“HEET si mradi wa majengo pekee, bali ni chombo cha mageuzi ya elimu ya juu kinacholenga kuzalisha wahitimu wabunifu, waadilifu na wenye ujuzi wa kuchochea uchumi wa viwanda,” amesema Profesa Anangisye.

Profesa Anangisye amebainisha kuwa kupitia mradi wa HEET, UDSM imepiga hatua kubwa ambapo utekelezaji umefikia zaidi ya asilimia 80.
Amesema mradi huo umewezesha ujenzi wa kampasi mpya katika mikoa ya Lindi (Ngongo na Ruangwa) na Kagera, pamoja na majengo 11 mapya ya kufundishia, hosteli, ofisi, kituo cha huduma za jinsia na mahitaji maalumu, pamoja na ukarabati wa majengo ya zamani katika Ndaki ya Uhandisi na Teknolojia (CoET).

Aidha, mradi wa HEET umewezesha chuo kufanya mapitio ya mitaala 250 ili iendane na mahitaji ya soko la ajira na maendeleo ya viwanda.
Ameongeza kuwa zaidi ya wanafunzi 39,000 na Wahadhiri 600 wananufaika na mfumo wa masomo kwa njia ya mtandao (e-learning), hatua inayoiweka UDSM katika nafasi ya kinara wa mageuzi ya kidijitali katika elimu ya juu nchini.

Kupitia ufadhili wa mradi wa HEET, UDSM pia imefadhili wanataaluma 29 kusomea Shahada za Uzamivu na Umahiri katika vyuo vikuu vinavyotambulika kimataifa ili kuongeza ubora wa utafiti na ufundishaji.

Vilevile, zaidi ya Kampuni 24 zimesaini makubaliano ya ushirikiano na chuo hicho, yakitoa nafasi za mafunzo kwa vitendo kwa wahitimu na Wahadhiri

