NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) inamshikilia Shaban Adam (54) mkazi wa jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kutengeneza dawa za kulevya aina ya Heroini.
Mtuhumiwa huyo alikamatwa nyumbani kwake Manzese Kilimani Juni 11, 2024 akitengeneza dawa za kulevya alizozitambulisha kama heroini kwa kutumia dawa tiba zenye asili ya kulevya akichanganya na kemikali bashirifu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam le Julai 17,2024 , Aretas Lyimo amesema mtuhumiwa huyo baada ya kutengeneza dawa hizo husafirisha kwa kutumia mabasi ya abiria kama vifurushi kwenda mikoa mbalimbali chini.
Amesema mtuhumiwa huyo ameieleza mamlaka hiyo kuwa, siku za nyuma alikuwa akitengeneza dawa hizo za kulevya katika nchi za bara la Asia kwenye magenge ya wazalishaji wa dawa za kulevya na pia alitumika kama mbebaji wa dawa hizo (punda) na aliporejea hapa chini aliendelea na uhalifu huo.
“Huyu mtengenezaji amekuwa akifanya hivyo baada ya kuadimika kwa dawa ya heroin ambayo tumefanikiwa kudhibiti, anachanganya vitu mbalimbali kwa kutumia dawa tiba ambazo zinatumika kutibu magonjwa kama kansa, moyo, lakini dawa zingine anazotumia zimekwisha muda wake,” amesema
Aidha amesema katika tukio jingine Mamlaka hiyo inamshikilia mtu mmoja aliyetambulika wa jina la Mbaba Issa mwenye hati ya kusafiria (Passpoti) namba TAE442718, ambaye alikamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Melchior laye Bujumbura Burundi akiwa na kiasi cha Kilogramu 3.8 za dawa za kulevya aina ya Skanka.
Lyimo amesema dawa hizo zilikuwa zimefichwa na kushonewa ndani ya begi la nguo na kwamba mtuhumiwa huyo alikamatwa akijiandaa kusafiri kuelekea Dubai.
“Kufuatia mikataba ya kikanda na kimataifa iliyosainiwa na Tanzania katika udhibiti wa dawa za kulevya, mhalifu yeyote wa dawa za kulevya atakaefanya uhalifu katika nchi zilizoingia makubaliano na kukimbilia moja ya nchi hizo atakamatwa,” amesema